Msafara wa magari ziara ya mkuu wa mkoa wa Ruvuma, ukiwa umekwama katika kijiji cha Mahenge wilayani Mbinga mkoani humo, wakati ukielekea leo katika kata ya Litembo. |
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
DIWANI
wa kata ya Litembo wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, kupitia tiketi ya Chama Cha
Mapinduzi (CCM) Altho Hyera amemtuhumu Meneja wa wakala wa barabara Tanzania
(TANROADS) mkoani humo, Abraham Kissimbo kwamba amekuwa kiongozi mwenye kauli
zisizoridhisha ambazo hazionyeshi uadilifu kama mtumishi wa umma.
Hyera
alisema hali hiyo ilimkuta wakati alipokwenda ofisini kwake kupata ufafanuzi
juu ya maendeleo ya ujenzi wa barabara yenye kilometa 26 kutoka Mbinga mjini
kwenda Litembo, ambayo hivi sasa ina hali mbaya kutokana na magari kushindwa
kupita katika kipindi hiki cha masika.
Diwani
huyo alimnyoshea kidole Injinia Kissimbo mbele ya Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Said
Mwambungu, kwenye mkutano wa hadhara wa wananchi uliofanyika katika kata hiyo.
Mkuu
huyo wa mkoa leo alikuwa katika ziara yake ya kikazi kutembelea kata ya Litembo
kwa lengo la kujionea kero hiyo ya barabara ambayo malalamiko yake yamedumu kwa
miaka mingi.
Alieleza
kuwa Injinia huyo alikuwa akimweleza kwamba barabara hiyo hawezi kuishughulikia
kwa sababu haina hadhi na kwamba zipo barabara ambazo hata kama
akiamshwa usiku wa manane atazipatia kipaumbele.
“Mheshimiwa
Mkuu wa mkoa Meneja wa TANROADS alikuwa akiniambia kwamba, “barabara hii hawezi
kuishughulikia kwa sababu haina hadhi, zipo barabara ambazo hata akiamshwa
usiku wa manane yupo tayari kuzipatia kipaumbele”, alisema Hyera.
Kwa
upande wake Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Mwambungu
aliagiza barabara hiyo kufanyiwa matengenezo haraka huku akifafanua kwamba
mkandarasi wa kuifanyia matengenezo tayari amekwisha patikana.
“Barabara
hii naagiza iimarishwe ijengwe kwa kiwango kinachotakiwa, nataka wakati wote
masika na kiangazi magari na wananchi wapite bila shida”, alisema Mwambungu.
Awali
wakati magari ya msafara wa Mkuu huyo wa mkoa yakielekea katika kata hiyo ya Litembo
majira ya asubuhi ulikumbwa na matatizo, baada ya magari hayo kukwama kwa muda
wa saa moja katika kijiji cha Mahenge kilichopo katani humo kutokana na
barabara hiyo inayolalamikiwa kuwa na hali mbaya.
Hata
hivyo ililazimika watu waliokuwa ndani ya magari hayo kushuka na kupisha
madereva, kufanya kazi ya kuyanasua ili yaweze kupita katika eneo hilo korofi na baadaye
kuendelea na ziara.
No comments:
Post a Comment