Monday, February 17, 2014

WAZAZI WILAYANI MBINGA WASHAURIWA KUPELEKA WATOTO WAO KATIKA CHUO CHA UFUNDI PILIKANO

Kibao kikionyesha mwelekeo wa chuo cha ufundi Pilikano, ambacho kipo umbali wa kilometa 18 kutoka Mbinga mjini mkoani Ruvuma.

Wanafunzi wakijifunza ufundi wa umeme wa majumbani.

Baadhi ya wanafunzi wakiwa darasani wakijifunza fani ya ushonaji.

Mkurugenzi wa chuo cha ufundi Pilikano, Bruno Kapinga, akizungumza na mwandishi wa habari hizi (Hayupo pichani) wakati wa mahojiano yaliyofanywa juu ya maendeleo ya chuo hicho. (Picha zote na Gwiji la matukio Ruvuma)



Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

WADAU wa elimu wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, wametakiwa kuwa na mwamko wa kupeleka watoto wao katika vyuo vya ufundi hususani kwa vile ambavyo vipo karibu na maeneo yao, ili waweze kupata ujuzi wa aina mbalimbali.

Aidha imeleezwa kuwa watoto wanaomaliza darasa la saba wilayani humo, wamekuwa wengi wakizurula mitaani hivyo ni vyema sasa wakapelekwa katika vyuo hivyo ili waweze kuwa na maendeleo katika fani za ufundi kwa faida ya kizazi cha sasa na baadaye.

Wito huo ulitolewa na Mkurugenzi wa chuo cha ufundi Pilikano Bruno Kapinga, kilichopo katika kata ya Mkumbi wilayani Mbinga wakati alipokuwa akihojiwa na mwandishi wa habari hizi juu  ya maendeleo ya chuo hicho.

Kapinga alisema kuwa chuo hicho kimesajiliwa na VETA na kilianza rasmi kutoa mafunzo ya ufundi mwaka 2012 katika fani ya ushonaji, magari na umeme.

Mkurugenzi huyo alisema kwamba wazo la kujenga chuo alilipata baada ya kupata ufadhili kutoka Uholanzi, ambapo wafadhili kutoka katika nchi hiyo waliweza kumsaidia vifaa vya ufundi katika fani hizo.


Kadhalika aliushukuru uongozi wa halmashauri ya wilaya hiyo kwa kumpatia ushirikiano mzuri wa mawazo na ushauri, hasa katika kipindi ambacho alikuwa na mawazo ya kuanzisha chuo hicho cha ufundi.

Alisema changamoto anayokabiliana nayo sasa ni Wazazi kutoka katika maeneo mbalimbali wilayani Mbinga, kutokuwa na mwamko wa kupeleka watoto wao hususani kwa wale wanaomaliza darasa la saba ambao wameshindwa kuendelea na masomo ya kidato cha nne, kwenda kujifunza fani mbalimbali katika hicho.

“Hapa changamoto kubwa ninayokabiliana nayo ni wazazi kutokuwa na mwamko wa kuleta watoto wao waweze kusoma katika chuo hiki, ni vyema Watanzania wote hususani ndugu zangu wa hapa Mbinga watuletee watoto wao waweze kujiunga na hapo baadaye wataweza hata kujiajiri wao wenyewe kupitia ujuzi watakaoupata kutoka hapa kwetu”, alisema Kapinga.

Hata hivyo alieleza kuwa mikakati aliyonayo kwa lengo la kukiendeleza chuo cha Pilikano, ataanzisha fani za kilimo na mifugo ili hapo baadaye kuweza kupata wataalamu wa kutosha kutoka katika fani hizo watakaoweza kueneza ujuzi wao kwa wakulima, katika masuala ya ujasirimali.

No comments: