Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
HALI si shwari katika mji wa Mbinga mkoani
Ruvuma, kufuatia kuanza kwa mgomo usio na kikomo wa wafanyabiashara
kama njia ya kufikisha ujumbe kwa Waziri wa viwanda na biashara
na serikali ya Rais Jakaya Kikwete, juu ya
gharama za mashine za kutolea risiti (EFD) wakidai kwamba gharama hizo ni kubwa
na ni sawa na kumtishwa mzigo mfanyabiashara ambao hauna tija kwake.
Mgomo huo umeanza leo asubuhi hii huku makundi ya wafanyabiashara wakiwa
wamekusanyika katika maeneo mbalimbali ya mji huo, huku wakipanga kufanya
maandamano kuwaadhibu wenzao wanaokiuka mgomo huo ambao wataonekana
wamefungua maduka.
Hali kwa upande wa wakazi wa Mbinga mjini na wale wa maeneo ya
vijijini ambao wanakuja kwa ajili ya
kupata huduma mbalimbali imewafanya wawe katika wakati mgumu kutokana na mgomo
huo, hivyo kujikuta wakiambulia makufuri katika maduka hayo.
Wafanyabiashara hao wametoa onyo kwa wenzao iwapo watafungua maduka yao watakiona cha moto na kuanzia wakati wowote sasa, wataanza msako wa duka moja hadi jingine kwani wamesema mgomo huo ni wa nchi nzima na wao wametii uamuzi wa wafanyabiashara wenzao katika mikoa yote iliyopo hapa nchini.
Mkuu wa wilaya ya Mbinga Senyi Ngaga alipotafutwa na mwandishi wa
habari hizi kwa njia ya simu, ili aweze kuzungumzia suala hilo alisema wapo
kwenye kikao wanajadili tatizo hilo hivyo atalitolea taarifa baadae.
“Hivi sasa nipo kwenye kikao tunajadili suala hili naomba nitafute
baadae kidogo tutaweza kuzungumza”, alisema.
Hata hivyo hadi habari hizi zinaingia mitamboni bado hali ilikuwa tete
ambapo makundi ya wafanyabiashara wa aina mbalimbali katika mji wa Mbinga,
yalikuwa bado yakiendelea kuonesha msimamo kwamba hawataweza kufungua maduka
yao wakidai kwamba wanapinga gharama kubwa za mashine hizo za kutolea risiti
huku wakiongeza kuwa ni vyema serikali, ikasikiliza kilio chao na kukifanyia
kazi kwa kupunguza gharama hiyo.
No comments:
Post a Comment