Na Kassian
Nyandindi,
Mbinga.
JESHI la Polisi wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, limefanikikwa
kumkamata Roster Ndunguru mkazi wa kijiji cha Mbangamao wilayani humo ambaye anadaiwa kuwa ni jambazi sugu na amekuwa
akifanya matukio mengi ya kiuhalifu ikiwemo kuwajeruhi watu na kunyang’anya
mali zao.
Aidha Jambazi hilo lilikuwa likitafutwa kwa muda mrefu baada
ya kumjeruhi Mratibu elimu kata ya Mbangamao, Florence Kowelo kwa kumjeruhi sehemu
mbalimbali za mwili wake na kumpiga na kitu kizito kichwani.
Tukio hilo imeelezwa kuwa lilitokea majira ya usiku wakati
Mratibu huyo akiwa nyumbani kwake amelala na familia yake, ambapo baada ya
kupiga kelele majirani walijitokeza na jambazi hilo lilitokomea kusikojulikana.
Kwa mujibu wa chanzo cha uhakika kutoka Jeshi la Polisi
wilayani Mbinga ambacho hakikutaka jina lake litajwe katika mtandao huu, kilisema kuwa
Roster amekuwa na matukio mengi ya kiujambazi ambayo amekuwa akiyafanya katika
maeneo mbalimbali wilayani humo.
Alisema amekuwa akitembea nyakati za usiku na silaha kama
vile panga, nondo ambavyo amekuwa akivitumia kujeruhi watu kisha kupora mali
zao.
Pamoja na mambo mengine alifafanua kuwa mafanikio ya kuweza
kumkamata yalitokana na jeshi hilo kupata taarifa kutoka kwa raia wema kwamba
jambazi hilo, lilikuwa likiranda randa katika kijiji cha Mbangamao wilayani
humo ndipo polisi walikwenda huko majira ya usiku wa Februari 20 na kuweza
kufanikiwa kumkamata.
Hata hivyo kaimu Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Ruvuma,
Revocatus Malimi alipotafutwa ili aweze kuzungumzia juu ya tukio hilo hakuweza
kupatikana na kwamba Jambazi hilo limelazwa katika hospitali ya wilaya hiyo, akiugulia
majeraha baada ya kuambulia kipigo wakati akijaribu kutoroka mikononi mwa Polisi.
No comments:
Post a Comment