Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
WASHIRIKI wa mafunzo ya kutengeneza
vito vya thamani wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, wameiomba serikali wilayani
humo kuendelea kuunga mkono mafunzo waliyoyapata ili yaweze kuleta faida kwa
kizazi cha sasa na kijacho.
Kauli hiyo ilitolewa kupitia risala
yao iliyosomwa na mmoja kati ya washiriki hao, Editha Komba mbele ya mgeni
rasmi Mkuu wa wilaya hiyo Senyi Ngaga wakati wa kufunga mafunzo hayo ya wiki
mbili yaliyofanyika katika chuo cha maendeleo ya wananchi (FDC) kilichopo mjini
hapa.
Aidha katika risala hiyo washiriki
hao walisema wameweza kujifunza kutengeneza ukataji wa vipande vya aluminiamu
na shaba, kutengeneza mapambo mbalimbali kama vile heleni, cheni na bangili.
Walieleza kuwa wameweza kujifunza kutumia
vitu vya asili kama vile mbegu za maembe, kahawa, maboga na manyoya ya kuku
kutengeneza mapambo ya asili.