Na Amon Mtega,
Songea.
WAFUASI wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na CHADEMA ambao
walijeruhiana katika mkutano wa mwisho wa kampeni za uchaguzi, kuwania nafasi
ya udiwani kata ya Mletele iliyopo manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, na kulazwa
katika Hospitali ya Songea [HOMSO] sasa wanaendelea vizuri baada ya afya zao
kuanza kurejea katika hali ya kawaida.
Mganga mkuu mfawidhi wa hospital hiyo Dkt.
Benedick Ngaiza alisema hayo wakati alipokuwa akizungumza na mwandishi wa
habari hizi.
Dkt. Ngaiza alisema katika watu waliojeruhiwa wanne
walitibiwa na kuondoka na waliokuwa wamelazwa walikuwa watatu ambao mpaka sasa
bado wanaendelea na matibabu ambapo mmoja ni Mashaka Mbawala [45] aliumizwa mikononi
na kichwani.
“Kwa mgonjwa aliyekuwa na jeraha la kusababishwa na
kitu chenye ncha kali inatakiwa uwangalizi wa karibu hata kama hali yake
inaendelea vizuri”
“Hivyo hata wakipata bahati ya kuruhusiwa bado
wataendelea kuangaliwa ili kubaini kama kunatatizo jingine linalo jitokeza”, alisema
Dkt. Ngaiza.
Majeruhi hao walijeruhiana Oktoba 27 mwaka huu majira
ya saa tisa mchana wakati wafuasi hao wakiwa kwenye mkutano wa mwisho wa
kufungia kampeni za uchaguzi mdogo kuwania nafasi ya udiwani katika
kata ya Mletele iliyopo manispaa ya Songea.
Pamoja na patashika hilo CCM iliibuka mshindi kwenye
kinyang’anyiro hicho kwa mgombea Maurus Lungu kushinda katika nafasi hiyo.
No comments:
Post a Comment