Tuesday, October 30, 2012

TATIZO LA MAJI SONGEA ALAUMIWE NANI?

Baadhi ya wakazi wa Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma wakiwa kwenye foleni wakisubiri kuchota maji, hivi sasa tatizo la maji katika Manispaa hiyo imekuwa ni kero kubwa ambapo upatikanaji wake ni wa shida. (Picha kwa hisani ya Demasho blog).

 

 
Na Kassian Nyandindi,
Songea.

UPATIKANAJI wa maji safi na salama ni tatizo ambalo limekuwa likiitesa jamii katika maeneo mbalimbali hapa nchini, na kusababisha hata maendeleo husika kurudi nyuma.

Maji ni kitu muhimu ambacho kiumbe chochote kilicho hai hapa duniani, hutegemea kuendesha maisha yake ya kila siku kwa kutumia nishati hiyo muhimu na ndio maana wananchi husisitizwa kutunza vyanzo vya maji ili visiweze kupotea.

Ni jambo la kushangaza kuona watu wanaendesha shughuli za kilimo katika vyanzo hivyo, huku viongozi husika wakikaa kimya na kuwaangalia bila kuchukua hatua stahiki, ambayo itaweza kukomesha hali hiyo.

Binafsi napenda kuelezea tatizo la upatikanaji wa maji safi na salama katika manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, ambapo takribani ni miezi miwili sasa imepita, wakazi wa manispaa hiyo wamekuwa wakikabiliwa na tatizo la upatikanaji wa maji na kulazimika kuyatafuta umbali mrefu.

Tatizo hilo linasababishwa na uzembe uliofanywa na wakazi wa manispaa hiyo kutokana na kuharibu vyanzo vya maji katika milima ya Matogoro na maeneo mengine kuzunguka mji wa Songea.

Licha ya manispaa hiyo kuwepo viongozi na mamlaka husika za kusimamia maji safi na taka (SOUWASA) hali imekuwa tete, ambapo kero hiyo inazidi kuwa kubwa kadiri siku zinavyosonga mbele.

Lawama zimekuwa zikielekezwa kwa wataalamu husika kutokana na kuzembea kusimamia kikamilifu utunzaji wa vyanzo hivyo vya maji, ambavyo ndio tegemeo kuu la kuzalisha maji katika mji huo.

Hali ya vyanzo imekuwa mbaya kutokana na kuanza kupoteza maji na vingine kukauka, na hili linatokana na baadhi ya wananchi kuendesha shughuli za kilimo, kulisha mifugo na ukataji wa miti ovyo.

Nionavyo uzembe huu umefanywa na viongozi husika kutokana na kile kinachodaiwa kwamba kushindwa kusimamia majukumu yao ipasavyo, kutokana na kuwaacha wananchi wakiendesha shughuli hizo zisizo rasmi katika vyanzo hivyo.

Binafsi natambua manispaa ya Songea ina mamlaka husika za kusimamia suala hili, hivyo sasa lawama zielekezwe kwao na ikiwezekana wahusika wachukuliwe hatua kwa kutowajibika ipasavyo katika majukumu yao ya kazi.

Upandaji wa miti katika vyanzo  vya maji ni suala la lazima na sio hiyari, hili kwa Songea ni aibu au fedheha kwa viongozi kutoshiriki kikamilifu kusimamia vyanzo hivyo hadi mwananchi anafikia hatua ya kuviharibu.

Uchomaji wa moto misitu imekuwa suala la kawaida hapa Ruvuma, kwa nini tusichukue hatua ya kudhibiti matatizo haya, maofisa misitu tunafanya kazi gani?

Sitakosea nikisema yatupasa tuwajibike katika hili kwa kuchukua hatua za haraka kunusuru hali hiyo ili jamii isiendelee kuteseka kama inavyo taabika sasa.

Ni jambo la kusikitisha ndoo ya maji katika mji huo inauzwa kwa shilingi 500 kutokana na maji hayo kutafutwa umbali mrefu na kuyaleta mjini kwa ajili ya matumizi ya binadamu.

Nimeshuhusdia nyumba za kulala wageni imekuwa ni kero kubwa juu ya upatikanaji wa maji, ambapo baadhi yake wageni wamekuwa wakizikimbia au kutoweka kabisa kutokana na ukosefu wa nishati hiyo muhimu.

Hii ni aibu….. ukizingatia kwamba mamlaka ya maji safi na taka ipo, na siku zote tumekuwa tukiona viongozi wake wakiwa maofisini wakifanya kazi na kutupatia taarifa nzuri kwamba vyanzo vyetu vya maji vimeboreshwa kwa kupandwa miti ili kuepukana na matatizo ya upatikanaji wa maji.

Zama hizi ni za uwazi na ukweli, hatuhitaji kudanganywa au kupewa porojo, ambapo mwenye macho haambiwi tazama, endapo kama taarifa hizi zingekuwa na ukweli kama huo ambao mmekuwa mkitupatia kutoka kwenye mafaili yenu leo tatizo hili lisingetukumba sisi wanasongea, nasema tumechoka kudanganywa tunachohitaji sasa tuone utekelezaji kwa vitendo ili adha hii tuweze kuondokana nayo.

Nauliza, kwa nini wananchi wale wanaoharibu vyanzo hivyo tunawafumbia macho kwa kutowachukulia hatua za kisheria hadi tatizo hili linafikia hatua ya kuwa kubwa? Majibu ya hili tatizo kila mmoja wetu anayo.

Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Bw. Said Mwambungu, Songea ni makao makuu ya mkoa huo, ni vyema uingilie kati suala hili ili uweze kunusuru maisha ya wananchi wako ambapo bila maji uhai wa binadamu yeyote yule hauwezi kusonga mbele.

Nashauri hivi sasa tunaelekea kipindi cha masika, hivyo miti kwa haraka na umakini ipandwe katika maeneo yaliyoathiriwa, ili kurudisha uto wake wa asili na kuhakikisha wale wananchi wanaoendesha shughuli za kilimo na kukata miti ovyo wanachukuliwa hatua za kisheria, ili tuweze kudhibiti na iwe fundisho kwa wengine wenye tabia kama hiyo.

Tusipo fanya hivyo tatizo hili litaendelea kuwa sugu na kusababisha hata magonjwa ya tumbo ambayo yapo sasa kuendelea kutesa watu kutokana na ukosefu wa maji safi na salama.

















 



No comments: