Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. (Picha na mtandao)
Na Dustan Ndunguru,
Songea.
PADRE wa kanisa la Roman Katoliki Bw. John Chacha
ambaye pia ni makamu mkuu wa chuo kikuu cha SAUT tawi la Songea mkoani,
ameshangazwa na baadhi ya watu ambao wanaobeza kazi zilizofanywa na
hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, kwa kusema hazikuwa na tija
katika Taifa hili.
Kauli hiyo aliitoa wakati wa
mahubiri ya ibada ya jumapili ambayo ilikuwa ni siku ya watakatifu waliyoishi
kwa uadilifu kwa kumcha Mungu, pamoja na utii mbele ya jamii ambayo iliyokuwa
ikiwazunguka.
Akihubiri katika kanisa la mtakatifu
Mathias Mlumba Kalemba jimbo kuu la Songea Padre Chacha alisema, kumekuwa na
tabia iliyozoeleka kwa baadhi ya watu kubeza kazi zilizofanywa na waasisi wa
nchi ambao walikuwa wanajituma usiku kucha kuhakikisha taifa linakwenda
sawa bila upendeleo.
“Ninashangazwa sana
kuona baadhi ya watu wamekuwa wakibeza kazi zilizofanywa na mwalimu Nyerere,
pamoja na wenzake na kusema kuwa suala la ufisadi lilikuwepo tangu enzi
za mwalimu jambo ambalo ni ukosefu wa fikra za kichambuzi na uwiano wa
kihistoria”
“Kwa kumbukumbu yangu mwalimu
Nyerere aliwahi kugoma kujengewa nyumba akasema kwa vile napenda kusoma vitabu
na maktaba yangu imechakaa naomba mnitengenezee, ili vitabu vyangu vikae sehemu
nzuri, lakini kwa mtanzania wa sasa akiambiwa hivyo tu ndio wa kwanza
kufuatilia ahadi hiyo bila hata kuwa na uwoga wowote”, alisema Padre huyo.
Alisema watanzania wa sasa
wanatakiwa kufuata mambo mazuri yaliyofanywa na mwalimu ambapo kwa kufanya
hivyo kila mtu atakuwa na uchungu na nchi yake na kuondokana na ubinafsi ambao
unaonekana kutawala kila mahali.
Padre Chacha alisema kila kiongozi
wa chama cha siasa na wanachama wake kwa ujumla, wanapaswa kujifunza kwa dhati
yale ambayo yalionyeshwa na waasisi na kwamba waache chokochoko ambazo siku
zote zinaonesha kutaka kuharibu amani na utulivu uliodumu kwa miaka mingi sasa.
No comments:
Post a Comment