Wednesday, October 31, 2012

WANANCHI WATAABIKA NA MAISHA

Kijiji cha Lunyere, kwa jina maarufu DarPori ambacho kipo umbali wa kilometa 98 kutoka Mbinga mjini, Ruvuma. Kijiji hiki kipo mpakani mwa Tanzania na Msumbiji wananchi wameilalamikia serikali kwa kushindwa kutengeneza barabara ya kutoka Mbinga mjini hadi huko, hali ya maisha yao ni mbaya kutokana na kukosa hata huduma za matibabu kama vile kituo cha afya au zahanati hakuna, tokea kijiji hicho kianzishwe mwaka 1992 na kusajiliwa rasmi mwaka 2003.(Picha na Kassian 
 Nyandindi)

Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
 
TUNAISHI kwa taabu serikali haitujali au kwasababu sisi tunaishi mpakani, miundombinu ya barabara kutoka Mbinga mjini kuja huku ni shida tupu, kilio chetu ni huduma za afya, maji na barabara.
 
Haya ndiyo maneno ya wakazi wa kijiji cha Lunyere kitongoji cha Darpori, wanaoishi katika kijiji hicho ambacho kipo umbali wa kilometa 98 kutoka Mbinga mjini.
 
Kijiji hicho kipo mpakani ambapo kinapakana na nchi ya Msumbiji upande wa Kusini na maisha kwenye kijiji hicho ambacho kipo mbali kuliko vyote katika Wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma , wananchi wake ni mchanganyiko wa makabila mbalimbali ambao hujishughulisha na kilimo, ufugaji, biashara na uchimbaji wa madini aina ya dhahabu.
 
Wakazi katika kijiji cha Lunyere wapo jumla 6060 Wanaume 3039 na Wanawake 302, hawana kituo cha kutolea huduma za afya, barabara zimekuwa mbaya na huduma ya maji kwao imekuwa ni shida.
 
Kwa mtu yeyote ambaye sasa anahitaji kwenda katika kijiji hiki ni lazima uumize kichwa kwanza, kwasababu vyombo vya usafiri kama magari hata pikipiki endapo ikinyesha mvua tu hasa kipindi hiki cha masika, huwezi kwenda huko hadi uhakikishe jua liwake na ardhi iwe imenyauka kidogo hapo utapata unafuu wa kwenda huko lakini kwa taabu na mateso makubwa.
 
Barabara yake kutoka Mbinga mjini hadi kijiji cha Mpepo ni nzuri, lakini kuanzia hapo hadi huko kijijini ni mbaya sana ina mashimo makubwa na hili linatokana na tokea kijiji hicho kianzishwe, mwaka 1992 na kupewa hati ya usajili mwaka 2003 serikali haijawahi kuifanyia matengenezo.
 
Asili ya barabara hiyo imetengenezwa kwa nguvu za wananchi kwa kutumia jembe la mkono, hivyo hakuna budi kwa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga na serikali kwa ujumla kuangalia upya namna ya kuiboresha, ili isiendelee kuleta adha kubwa kwa wananchi kama wanavyoipata sasa.
 
Kadhalika kijiji hicho tokea kianzishwe hakina zahanati au kituo cha afya  ambacho kingewawezesha wananchi kupatiwa matibabu, hivyo kutokana na wao kuishi mbali na kukosa huduma hiyo muhimu watu wengi wamekuwa wakipoteza maisha.
 
Tegemeo lao kubwa pale wanapohitaji matibabu huenda kununua dawa katika duka moja la dawa muhimu ambalo lipo kijijini hapo, na mgonjwa anapozidiwa, hubebwa kwa kutumia machela kwa kutembea umbali  wa kilometa 20 hadi kituo cha afya kilichopo katika kijiji cha Mpepo kutafuta huduma za matibabu.
 
Tatizo hili la kufuata huduma hiyo muhimu linasababishwa na magari kwenda huko kwa nadra kutokana na barabara kuwa mbaya.
 
Mbaya zaidi wagonjwa wengi hufia njiani hasa kwa wale ambao wanakipato cha chini au wale ambao hawana hata ndugu wa kuwatunza.
 
Wengine hufariki kutokana na kukosa msaada utakuta maiti zao huhifadhiwa katika ofisi ya Mtendaji wa kijiji hicho cha Lunyere, zikisubiriwa kupatiwa msaada wa mazishi.
 
Nimezungumza na mtendaji wa kijiji hicho Bw. Raphael Mapunda anasema muda mwingi anakuwa katika wakati mgumu, kutokana na kijiji kukosa hata zahanati au kituo cha afya cha kutolea huduma ya tiba ili wananchi wake wasiendelee kuteseka.
 
Anasema jambo hilo hivi sasa limemfanya kuweka mipango madhubuti ya kuhamasisha wananchi kuanzisha mfumo wa kutoa michango ambayo ifikie zaidi ya milioni 40 ili waweze kuanza kujenga kituo cha afya.
 
Anasema kwa kila mwezi jumla ya watu watano hufariki dunia na maiti hutelekezwa katika ofisi yake, hivyo uongozi wa kijiji hicho hupata shida mara kwa mara kuchukua jukumu la kwenda kuzika maiti ambazo hutelekezwa ofisini hapo.
 
Nimemuuliza kwa nini watu wamekuwa na mazoea ya kutelekeza maiti ofisini kwake, ameniambia kwamba hili linatokana na serikali kutosikiliza kilio chao cha muda mrefu cha kuwajengea kituo cha kutolea huduma za afya.
 
Aidha huduma za maji zimekuwa zikipatikana kwa shida kutokana na mradi uliojengwa katika kipindi cha mwaka jana kwa ufadhili wa halmashauri ya Wilaya ya Mbinga kuwa chakavu, kwani mabomba ya maji ambayo yamefukiwa ardhini kupasuka mara kwa mara.
 
Binafsi nasema kuna umuhimu sasa kwa serikali na viongozi wa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga, kufanya kila liwezekanalo kuchukua hatua ya kunusuru maisha haya ya wakazi wa kijiji cha Lunyere kutokana na kilio chao kudumu kwa miaka mingi.
 
Wananchi wanaoishi huko wamekuwa ni walipa kodi kama wengine waliopo kwenye maeneo mengine hapa nchini, kwa nini leo hii wamesahaulika kiasi hiki utadhani kwamba hawana baba wala mama, hii ni dhambi na aibu kwa serikali hii ya awamu ya nne yenye kutamba kwa falsafa yake ya ari, nguvu na kasi mpya.
 
Mkazi mmoja wa kijiji hicho Bi. Anastazia Hashim anasema viongozi wengi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo wamekuwa wakiishia katika kijiji cha Mpepo, wakati wa kuwatembelea wananchi na wanaogopa kwenda kijiji cha Lunyere kutokana na barabara kuwa mbaya hasa katika kipindi hiki cha mvua nyingi ambazo hunyesha.
 
Utafiti uliofanywa na mwandishi wa makala haya umebaini hata hali ya maisha ya wakazi wa kijiji hicho imekuwa ni ngumu, bidhaa zimepanda bei kutokana na barabara kuwa mbovu, ambapo hata sukari kilo moja ni shilingi 3000 na nyama huuzwa kilo moja shilingi 8000 je, kwa hali hii mwananchi wa kawaida ataweza kuondokana na umasikini?.
 
Ugumu wa maisha na bidhaa kuwa bei juu kunasababishwa tu na tatizo la hali ya barabara ambapo hata migahawa inayouza vyakula hali imekuwa sio nzuri, gharama za vyakula zimekuwa mbaya kiasi ambacho mwananchi wa kawaida hawezi kumudu.
 
Hali kadhalika suala la ulinzi na usalama kwa wananchi hao wanaoishi mpakani mwa Tanzania na Msumbiji, imekuwa ni tete kutokana na kutokuwepo hata kituo cha polisi au maofisa uhamiaji kwani wageni wengi kutoka nchi hiyo jirani wamekuwa wakiingia kutoka kiholela bila kufuata taratibu husika.
 
Kitendo cha serikali kutokuwa makini na kuacha mianya hii ya raia wageni kuingia bila uwoga, ni hatari hapo baadaye hivyo yatupasa sasa tuondoke maofisini na kwenda kufanya upembuzi yakinifu juu ya kudhibiti tatizo hili ambalo baadaye litatugharimu.
 
Inadaiwa kwamba silaha zimekuwa zikiingizwa kienyeji kutoka huko Msumbiji na hao wageni, je tusipo kuwa makini katika hili tunajenga tabaka gani hapo baadaye?
 
Siku zote wahenga wetu husema ili uweze kulala ndani ya nyumba yako ukiwa salama na usishambuliwe na mnyama mkali kama simba, kwanza hakikisha unaimarisha ulinzi kwa kufunga milango na madirisha ndipo utaweza kulala usingizi mzuri, hivyo sasa tunyanyue nyayo zetu na kwenda huko kuweka ulinzi mzuri.
 
Kama kweli tuna nia madhubuti ya kuwatumikia wananchi, kulingana na kiapo tulichoapa wakati tunakabidhiwa madaraka tuliyonayo, si kweli eti viongozi mnashindwa kwenda huko hali hii itadumu mpaka lini siku zinazidi kwenda, tutumie busara sasa.
 

No comments: