Upande wa kulia katibu wa kikundi cha wavuvi wa samaki Mbamba bay Bw. Agrey Ngonyani, akionyesha aina ya nyavu ambazo hutumika kuvulia samaki. Kushoto ni mvuvi wa samaki Bw. Simon Lwela, wakiwa karibu na ziwa Nyasa.
Na Kassian Nyandindi,
Nyasa.
WANAFANYA
kazi za uvuvi kwa kutumia vifaa duni, wavuvi hupoteza maisha yao, waiomba
serikali kusikiliza kilio chao ili waweze kuondokana na matatizo
wanayokabiliana nayo.
Hawa
ni wananchi kutoka jamii ya wavuvi waishio katika mwambao mwa ziwa Nyasa wilaya
ya Nyasa, mkoani Ruvuma ambao tegemeo lao la kukuza uchumi katika maisha yao ya
kila siku ni shughuli za uvuvi.
Wamekuwa
wakivua samaki wa aina mbalimbali na dagaa ambao huuza na wengine hutumika kwa
kitoweo majumbani, pia wengine wamekuwa wakijishughulisha na kilimo cha zao la
mhogo, mpunga, mbogamboga na matunda.
Lakini
jitihada zao za uvuvi zinakwamishwa kutokana na kukosa zana za kisasa za uvuvi
na hii inatokana na wananchi wengi kutokuwa na uwezo wa kumudu gharama za
kununua maboti ya kisasa ambayo wangeweza kutumia kwa uvuvi.
Wameweza
kuunda umoja wao wa wavuvi uitwao Samaki Business, uliopo katika mji mdogo wa
Mbamba bay, na kusajiliwa mwaka 2009.
Umoja
huu umekuwa ukivua samaki aina ya katoga, kambale na dagaa nyasa ambao huuzwa
ndani na nje ya mkoa wa Ruvuma .
Bw. Agrey
Ngonyani ni Katibu wa umoja huo anasema samaki hao wanavua kwa mtindo wa kutega
nyavu kuanzia nchi nne na kuendelea.
Anasema
mikondo ya maji katika ziwa Nyasa imekuwa ya kasi hivyo wavuvi wanashindwa
kuvua kutokana na kuwa na vifaa duni ambapo wamekuwa wakitumia mitumbwi jambo
ambalo ni hatari kwa maisha yao .
“Wengi
tumekuwa tukipoteza maisha, kwa mwaka hujitokeza vifo vya wavuvi kufa maji,
visivyopungua watu watatu hadi wanne kutokana na uduni wa vifaa vyetu vya
uvuvi,
“Uvuvi
mwambao mwa ziwa hili ndio mama anaye tufanya tuishi, hata mzunguko wa fedha
unatokana shughuli hizi za uvuvi”, anasema.
Bw. Ngonyani
anasema wavuvi waliopo ni zaidi ya 100 katika kikundi chao hivyo wanaiomba
serikali iwasaidie vifaa vya kisasa vya uvuvi kama vile maboti ya kisasa na sio
kutumia mitumbwi kama ilivyo wanavyofanya sasa ambapo huwafanya washindwe
kutimiza mahitaji yao ya kuvua samaki wengi.
Anabainisha
kuwa kwa siku wamekuwa wakivua samaki tani 3 au zaidi na kuwahifadhi kwa mfumo
bora unaotakiwa tayari kwa kusafirishwa kwenda kuuzwa.
Changamoto
nyingine wanayokabiliana nayo ni kukosa meza za kuanikia ambapo kwa sasa
hutumia matete kutengeneza meza za kuanikia, tekinolojia ambayo imekwisha pita
na wakati.
“Tunaishukuru halmashauri yetu ya wilaya ya Mbinga, kutufikishia elimu sahihi ya uvuvi hivyo
wavuvi wengi unaowaona hapa elimu hii imewafikia na wanavua kwa kufuata
taratibu husika”, anasema Bw. Ngonyani.
Anaongeza
kuwa suala la mikopo kwao imekuwa ni shida hivyo wanaziomba taasisi mbalimbali
za kifedha kama vile mabenki kuwakopesha fedha ili waweze kuendesha umoja wao
wa wavuvi uitwao Samaki business.
Bi. Bupe
Kalikene ambaye anashughulika na uuzaji wa samaki na dagaa anasema, tatizo
wanalokabiliana nalo ni kukosa soko la uhakika katika mauzo ya samaki na dagaa.
Anasema
wamekuwa wakiuza kwa mtindo wa kuwasafirisha kwa marafiki zao na kupeleka
Mbinga mjini au Songea na baada ya siku kadhaa hurejeshewa fedha mara baada ya
mauzo kufanyika.
“Hakuna
soko la uhakika, hakuna wafanyabiashara wanaokuja kununua hapa moja kwa moja
bali tunafanya jitihada za kuuza sisi wenyewe”, anasema.
Baadhi
ya wavuvi wengine suala la kuwa na vitendea kazi duni huwafanya kutumia nguvu
kubwa katika shughuli hizo za uvuvi ili waweze kuuza na kupata fedha za
kujikimu kimaisha.
Mvuvi
Simon Lwena anasema samaki ni wengi katika ziwa Nyasa lakini wanashindwa
kuwavua kwa wingi kutokana na kukosa zana borab za kisasa.
Bw. Lwena
anasema hali hiyo inasababisha uhaba wa samaki ambapo wachache wanaopatikana
bei yake huwa juu na kusababisha hali ya maisha yao kuwa magumu kwa wavuvi na
wananchi wengine.
“Wakazi
wa wilaya hii ya Nyasa hususani hapa Mbamba bay tusingekuwa na maisha magumu
kama shughuli zetu za uvuvi zingekuwa zinafanywa kama maeneo mengine hapa
nchini kwa kutumia vifaa vya kisasa”, anasema Lwena.
Anasema
samaki hawa wa ziwa Nyasa ni wazuri na wanapendwa na watu wengi, kuna samaki wa
aina nyingi lakini wanashangaa kwa nini serikali inashindwa kutumia ziwa hilo
kama kivutio cha watalii na kufanya biashara kubwa ya samaki kama ilivyo katika
ziwa Victoria.
Pamoja
na mambo mengine anashauri kwa kuitaka serikali iwakopeshe mikopo ya fedha
kupitia vikundi vyao vya uvuvi vilivyosajiliwa kisheria ili waweze kununua zana
bora na hatimaye kuondokana na usumbufu wanaoupata sasa.
Ofisa
uvuvi wa mji mdogo wa Mbamba bay aliyejitambulisha kwa jina moja la Mwasaga anasema,
serikali inafanya utaratibu wa kuleta wataalamu wa kutengeneza maboti ya mbao
ambayo yatafungwa injini kwa ajili ya kuwarahisishia wavuvi kufanya shughuli
zao za uvuvi kwa ufasaha zaidi.
Bw. Mwasaga
anaongeza kuwa juu ya suala la wavuvi kupewa mikopo wanapaswa kufanya jitihada
zao za kuomba mikopo kupitia taasisi za kifedha ili waweze kuboresha shughuli
zao na sio kuitegemea serikali peke yake.
No comments:
Post a Comment