Na Steven
Augustino,
Tunduru.
BAADHI ya wakulima wa wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, wameitaka serikali kuwabana viongozi wenye tabia ya kujinufaisha matumbo yao kupitia pembejeo
za ruzuku ili wananchi waweze kuboresha mashamba yao katika msimu huu wa
kilimo.
Hayo yalisemwa na wadau mbalimbali waliohudhuria katika
mdahalo wa kukusanya maoni kupitia mdahalo wa kuwajengea uwezo juu ya utekelezaji
wa shughuli za sekta ya kilimo uliowahusisha wadau wa kilimo kutoka jimbo la
Tunduru Kaskazini uliofanyika ukumbi wa Skyway mjini hapa.
Kadhalika wakulima hao walishauri kwamba serikali iangalie uwezekano
wa kuondoa utaratibu wa kupeleka pembejeo hizo kwa wakulima wake na badala yake ihamasishe wawekezaji
kujenga viwanda vingi ili kuongeza uzalishaji na fedha hizo kuingizwa kama hisa
katika viwanda hivyo ili mbolea au mbegu ziuzwe kwa bei nafuu.
Wakifafanua wakati wa kuchangia maoni yao kwa nyakati tofauti
Bw. Sekula Matumla, Bw. Addo Makanya, Rashid Issaya, Halifa Chitemwe na Bi.
Sarra Mwingira walisema kuwa hali hiyo inatokana na viongozi wa halmashauri ya wilaya hiyo wakiwemo wawakilishi wao madiwani na wabunge, kutokuwa na mwamko wa kusimamia kikamilifu ugawaji wa pembejeo za ruzuku zinazotolewa na
serikali.
Walibainisha kuwa kwavile kikwazo cha maendeleo katika wilaya
ya Tunduru kinatokana na ubovu wa miundombinu ya barabara zao wakatumia nafasi
hiyo kuiomba serikali kuangalia uwezekano wa kukatisha mkataba na kuifukuza
Kampuni ya Progressive Higleig JV Contractors, iliyopewa mkataba wa kujenga barabara kwa
kiwango cha lami kilometa 189 kutoka wilayani Namtumbo hadi Tunduru mkoani humo, ambao ujenzi wake unasuasua hadi sasa.
Bw. John Luanda, Musa Komba na Athman Idd Milanzi walisema
kuwa kitendo cha viongozi hao kushindwa kuwajibika kwa wananchi ndiko kunako sababisha
vijana kuwa tegemezi kwa wazazi wao na kuwa na ulemavu wa kufikia hatua
ya kuzaa na kuacha watoto wao kwa bibi au babu zao kwa ajili ya
kulelewa wakati wao wakiwa wanatumia mtindo wa Nungunungu ambaye huchimba
udongo na kuurudisha nyuma.
Wakati hayo yakiendelea pia wakulima hao wakatumia nafasi
hiyo kuishauri serikali kuandaa utaratibu wa kuwakagua viongozi, ambao wamekuwa
wakijinufaisha kupitia mwamvuli wa vyama vya ushirika na kubuni mbinu za
makusudi kuhakikisha kuwa mikakati yake inafanikiwa.
Wachangiaji wengine ni pamoja na mwanafunzi wa shule ya
sekondari Mataka; Asha Mussa, Bi. Kassiana Magogwa, Bw. Mussa Ndeka na Mussa
Komba, Bi. Atingala Mohamed nao katika maoni yao waliishauri serikali kuufuta mfumo wa
stakabadhi ghalani kwa madai kuwa mfumo huo, unawafanya wakulima kulipwa malipo
yao zaidi ya mara moja hauna manufaa kabisa kwa zaidi ya kuwagandamiza huku wakilia
na utekelezaji mbovu unaofanywa na watendaji husika.
Wakulima waliendelea kudai kuwa kitendo cha serikali
kuendelea kupunguza idadi ya pembejeo zinazopelekwa kwa wanufaika yaani wakulima ni swan a kurudisha nyuma maendeleo katika
sekta ya kilimo.
Akizungumzia maudhui ya mdahalo huo Mwenyekiti wa
mtandao wa asasi za kiraia wilayani Tunduru(MATU) Bw. John Nginga alisema kuwa
pamoja na kukusanya maoni yatakayosaidia kuboresha huduma za kilimo, alikemea
pia tabia za wananchi kutohudhuria katika mafunzo kwa kikwazo cha
vikao visivyokuwa na posho.
Akifunga madahalo huo Mwenyekiti wa halmashauri ya Wilaya ya
Tunduru diwani Faridu Khamisi, pamoja na kuwapongeza wafadhili wa mdahalo huo ambao ulifadhiliwa na “The Foundation for Civil Society” aliwataka
maafisa ugani kuzitumia changamoto hizo kuboresha huduma zao kwa wakulima na
kutunza takwimu zitakazo wasaidia kukwepa vikwazo vya maendeleo.
No comments:
Post a Comment