Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Bw. Shaibu Nnunduma.
Na
Kassian Nyandindi,
Mbinga.
WAKAZI
wa kijiji cha Nyoni kata ya Nyoni Wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, wamelalamikia kitendo cha Halmashauri ya wilaya hiyo kutokarabati zahanati ya
kijiji hicho kwa miaka mingi iliyopita.
Bw. Dominicus
Kapinga mmoja kati ya mkazi wa kijiji hicho anasema hali ya zahanati hiyo sio
nzuri kutokana na kutelekezwa kwa miaka mingi, na kwamba kijiji cha Nyoni ni
moja kati ya vijiji maarufu wilayani humo ambavyo wakazi wake wameweza kupiga
hatua mbalimbali za kimaendeleo, katika kilimo cha mazao ya chakula na biashara
yaani kahawa na mahindi.
“Zahanati
yetu ya kijiji imetelekezwa miaka mingi, ukizingatia kwamba ni kijiji chenye
historia nzuri kutokana na hata Mwalimu Nyerere kutembelea hapa kuweka jiwe la
msingi katika ofisi ya chama cha mapinduzi tawi la Nyoni”, anasema Kapinga.
Wakati
huo huo nao wahudumu wa afya katika zahanati ya kijiji hicho na kituo cha afya
cha Myangayanga wilayani humo, wamelalamikia nyumba wanazoishi kuwa ni chakavu
zina hali mbaya jambo ambalo linahatarisha usalama wa maisha yao .
Wakizungumza
na mwandishi wa habari hizi kwa nyakati tofauti baada ya kutembelea katika maeneo hayo,
walisema nyumba hizo zinahatarisha usalama wa maisha yao hasa kipindi hiki cha
masika.
Nyumba
mbili za waganga katika kituo cha Myangayanga zimejenga nyufa kubwa huku kuta
zake zikiwa chakavu, na kwa zahanati ya Nyoni nyumba tatu wanazoishi waganga
nazo ni chakavu hazijafanyiwa matengenezo siku nyingi.
Katika
kijiji cha Nyoni mwandishi wa habari hizi ameshuhudia nyumba moja ya mganga
kati ya hizo tatu, ikiwa imeezuliwa na upepo mkali ambao uliambatana na mvua
kubwa, Januari 21 mwaka huu majira ya usiku, na kusababisha mganga aliyekuwa
akiishi humo kuondoka na kwenda kupanga uraiani.
Wafanyakazi
wanaoishi katika maeneo hayo wamekuwa wakipata shida kufuata maji umbali mrefu
mtoni, kwa ajili ya matumizi ya kwenye vituo hivyo na matumizi yao binafsi ya
nyumbani kutokana na maeneo hayo kutokuwa na miundombinu ya mabomba ya maji.
“Kwa
kweli tunapata shida, tunaamka usiku wa manane kutafuta maji umbali mrefu ni
vyema serikali isikilize kilo chetu na kumaliza kero hii mapema”, alisema
mganga wa zahanati ya Nyoni Imelda Ndunguru.
Naye
mganga mkuu wa kituo cha afya Myangayanga Bw. Athuman Songoro anasema kituo hicho
kinakabiliwa na upungufu mkubwa wa madawa na vitendea kazi katika kitengo cha
mama na mtoto ikiwemo hata akina mama wajawazito.
Bi. Esther
Nyika ni mhudumu wa afya wa kituo hicho naye anasema nyumba wanazoishi zinavuja
sana pale mvua zinaponyesha hivyo wanauomba uongozi wa halmashauri ya wilaya
hiyo kuangalia uwezekano wa kuzikarabati.
Nimeshuhudia nyumba mbili wanazoishi wafanyakazi hao wa kituo cha afya
Nyoni, zikiwa kama gofu ambalo limetelekezwa miaka mingi.
|
No comments:
Post a Comment