Saturday, November 24, 2012

SERIKALI YAOMBWA KUJENGA SOKO LA MAZAO TUNDURU


Na Steven Augustino,
Tunduru.

WAKULIMA  wa zao la korosho wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma wameiomba serikali  kuchukua hatua za haraka, kutatua kero ya kukosekana kwa soko la mazao wanayozalisha hali inayowafanya, kuuza mazao hayo kwa walanguzi wanaotumia kipimo
maarufu kwa jina la Kangomba, ili waweze kusukuma maisha yao ya kila siku.

Pamoja na malalamiko hayo wakulima hao walitumia nafasi hiyo kuishauri halmashauri ya Tunduru kupunguza ushuru wa mazao ambao umekuwa ukitozwa sasa kwa wakulima wake shilingi 200 kwa debe.

Kilio hicho kilipazwa na wakulima hao kupitia mdahalo wa mchakato wakukusanya maoni ya wananchi katika utekelezaji wa shughuli za sekta ya kilimo uliowahusisha wadau wa kilimo kutoka katika  Jimbo la Tunduru Kusini na kufanyika katika  ukumbi wa Skyway mjini hapa.

Bw. Said Kaisi, Asha Mussa, na Bw. Zacheus Kiyao, walisema kuwa kukosekana kwa utekelezaji na usimamizi wa mipango inayobuniwa na serikali kumekuwa kukiwakosesha imani wananchi kwa serikali yao na kuhisi huenda viongozi wao hawasimamii vizuri maendeleo husika.

Nao wawakilishi wa wakulima wa kilimo cha umwagiliaji(NAMASONYA) Bw. Rotari Komba, wakulima wa mazao ya nafaka (WAMANATU) Bw. Athumani Milanzi na mwakilishi wa kikundi cha walemavu(CHAWATA) wilayani humo Bi. Daria Haridi walisema kuwa kukosekana kwa masoko ya uhakika kwa wakulima wa mazao mbalimbali, kunawafanya wakulima kutafsiri kuwa kilimo ni kama adhabu kwao.

Walisema pamoja na hali hiyo serikali haina budi kuwatelekeza wakulima wake huku wakitumia nafasi hiyo kuishauri kuandaa utaratibu wa kutoa mikopo kwa kuwashindanisha wakulima bora, kuanzia ngazi za vijiji, Kata, tarafa, wilaya hadi ngazi ya mkoa na taifa kwa ujumla ili na wao waweze kuonja matunda hayo ya serikali, tofauti na sasa ambapo ni wafanyabiashara na watumishi pekee ndio wanaonufaika na mikopo hiyo kutoka serikalini.

Aidha wakulima hao pia wakatumia nafasi hiyo kwa kuendelea kupaza sauti na kilio chao, juu ya pembejeo za kilimo kuwa ghali pamoja na kutokuwepo kwa usimamizi mzuri wa viongozi kwa mgao wa upatikanaji wa Pembejeo za Ruzuku na kuwafanya wakulima hao kuitafakari Kauli  mbiu ya Kilimo kwanza kwa wilaya ya Tunduru kuwa ni Kilimo mwisho.

Awali akisoma risala ya mdahalo huo Katibu wa Mtandao wa Asasi za Kiraia wilayani Tunduru (MATU) Bw. Athumani Haji alisema, lengo la mdahalo huo uliofadhiliwa na “The Fondation for Civil Society” ni kukusanya maoni yatakayosaidia kuboresha huduma za kilimo ili kionekane kuwa cha kibiashara tofauti, na sasa ambapo mkulima mdogo amekuwa akiishia kupata mazao kwa ajili ya chakula nyumbani.

Alisema endapo mazingira hayo yataboreshwa kutakuwa kivutio kikubwa kwa kundi kubwa la vijana ambao wamekipa kisogo, kutokana na kuonekana kutokuwa na faida kwao.
 
Wawezeshaji wa mdahalo huo, Bi. Amina Nalicho na Bw. Andrew Tarimo waliwataka maafisa ugani kutumia mashamba darasa kutoa elimu kwa wakulima wote katika maeneo yao, ikiwa ni juhudi za serikali kuhakikisha kuwa wakulima wanapata mafanikio kupitia Kilimo.

‘’Pamoja na changamoto za uchache wa watumishi wa sekta ya kilimo uliopo, tumieni mashamba darasa kutoa elimu kwa wakulima wenu“, alisema Bi. Nalicho na kuongeza kuwa vinginevyo ajira zao za ubibi shamba na ubwana shamba hazitakuwa na maana endapo hakutakuwa na mafanikio kwa wakulima.

Aidha Bi. Nalicho alitumia nafasi hiyo kuwahimiza wakulima kutunza mazingira kwa kuacha kukata na kuchoma miti ovyo, kutolima katika maeneo ya vyanzo vya maji na kuwataka  wakulima kutumia vizuri nafasi zao katika uteuzi wa wanufaika wa pembejeo ili kuondoa migogoro na malalamiko yasiyo na msingi. .

Mkuu wa wilaya ya Tunduru Bw. Chande Nalicho pamoja na mambo mengine aliahidi kuendeleza ushirikiano na asasi za kiraia zikiwa ni juhudi za serikali kuhakikisha kuwa wilaya hiyo inapiga hatua katika nyanja za kimaendeleo ikiwemo kilimo.

Sambamba na hali hiyo serikali wilayani humo imewataka wananchi kushirikiana katika ulinzi wa amani na utulivu kwa kutoa taarifa za matukio ya uhalifu vinginevyo nadharia ya Kilimo kwanza haitaleta tija kwa wananchi wake.

Bw. Nalicho akatumia nafasi hiyo kuwahimiza wananchi wa wilaya hiyo ambayo inategemea kilimo kwa asilimia 95% ya wakazi wake kuwa wazitumie vizuri fursa zilizopo ili kujiletea maendeleo.

Wilaya hiyo yenye ukubwa wa eneo la hekta za mraba milioni 1.570,000  ambapo  eneo linalofaa kwa kilimo ni hekta 914,000 na kwamba kinachosikitisha ni kuwepo kwa takwimu ndogo ya eneo linalo limwa katika vipindi vya misimu ya kilimo cha mazao ya chakula na biashara.

Alifafanua kuwa takwimu hizo zinaonesha kuwa kati ya eneo hilo ni hekta 200,000 ndizo zinazolimwa sasa.
  

No comments: