Na Kassian
Nyandindi,
Mbinga.
WANANCHI wa jimbo la Mbinga Mashariki mkoani Ruvuma,
wametakiwa kuendelea kujituma katika shughuli mbalimbali za kimaendeleo ili
waweze kuondokana na umaskini, ambao umekuwa ukiitesa jamii miongoni mwao.
Mbunge wa jimbo hilo Bw. Gaudence Kayombo(Pichani) alisema hayo
wakati alipokuwa akizungumza na Mwandishi wa habari hizi, juu ya mikakati
mbalimbali ya kusukuma maendeleo katika jimbo lake.
Bw. Kayombo alisema kuwa anafurahishwa na wananchi wa
jimbo la Mbinga Mashariki, kwamba wengi wao wamekuwa wakijituma katika shughuli
za maendeleo hasa katika nyanja ya kilimo cha mazao mbalimbali.
Alisema hivi sasa amekuwa akihamasisha wananchi hao
kuunda vikundi vya kilimo cha mazao mchanganyiko yakiwemo mahindi, maharage
alizeti na mpunga lengo ni kuwafanya waweze kuwa na kipato ambacho kitawasaidia
hata kupeleka watoto wao shule.
“Hivi sasa tupo katika mchakato wa kusajili vikundi 60
vya mazao mchanganyiko changamoto niliyonayo sasa mwitikio ni mkubwa mno, na
mimi nimefurahishwa sana na wananchi wangu kupokea jambo hili kwa mikono miwili
hivyo usajili huu utakapokamilika tutafuta masoko ili waweze kuuza mazao yao
kwa bei nzuri”, alisema.
Alifafanua kuwa usajili wa vikundi hivyo utasaidia
hata kwa kikundi husika kiweze kutambulika kisheria serikalini na kwa taasisi
binafsi, zikiwemo benki ambazo zitaweza kuwapa mikopo ya kuendeshea shughuli zao
za kilimo.
Kadhalika aliongeza kuwa amekwisha fanya mawasiliano
na shirika la VECO na AGRI CORD yaliyopo Ubelgiji, kwa ajili ya kuweza kusaidia
vikundi vya kilimo cha mazao mchanganyiko wilayani Mbinga, kwa kuwapa utaalamu
wa kilimo bora na hata msaada wa kifedha kwa ajili ya kuendeshea shughuli za
kilimo.
Pamoja na mambo mengine, awali alieleza kuwa ameweza
kuhamasisha pia wakulima wa zao la kahawa wilayani humo, kuunda vikundi vya
wakulima wa kahawa ambapo jumla vipo 64 ambavyo vimesajiliwa kisheria na sasa
vimekwisha anza kazi ya kuuza kahawa yao katika msimu wa mwaka huu wa mavuno ya
zao hilo.
“Tumekwisha peleka tani 140 za kahawa zipo pale
Makambako kwa ajili ya kuuza mnadani, na mimi nimezungumza na watu wa Korea
kusini na Israel ambako kuna masoko makubwa wapo tayari kununua kahawa yetu,
kupitia vikundi hivi vilivyosajiliwa”, alisema Bw. Kayombo.
Hata hivyo alieleza kuwa kufikia mwaka 2014 katika
wilaya ya Mbinga kutajengwa kiwanda cha usindikaji wa kahawa, lengo likiwa ni
kukuza uchumi wa wilaya hiyo na taifa kwa ujumla.
“Nimeanza kuzungumza na wafadhili ambao watasaidia
katika ujenzi huu, kuanzia mwakani mwezi Januari watakuja kwa ajili ya kuanza
upembuzi wa awali juu ya kazi hii”, alisema.
No comments:
Post a Comment