Utafiti wa mbolea ya Minjingu Hyper pamoja na UREA |
Na Mwandishi wetu,
Mbinga.
WAKULIMA wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma
wameiomba serikali, kuwapelekea mapema pembejeo za kilimo(ruzuku) ili ziweze
kutumika kwa wakati ikilinganishwa na misimu iliyopita, pembejeo hizo zilikuwa
zikiwafikia kwa kuchelewa.
Wakulima wa kata ya Kihungu walisema kuwa kuchelewa kuwafikia kwa
mbolea hizo, kumekuwa kukiwaathiri na kusababisha washindwe kuzalisha mazao
mengi na hivyo kupata hasara.
Mkulima Aderick Komba alisema dhamira ya serikali ya kuwapatia
mbolea za ruzuku ni nzuri, lakini imekuwa ikikabiliwa na vikwazo vingi katika
usambazaji wake jambo ambalo mwisho wa siku humuumiza mkulima.
Bw. Komba alisema kuwa pamoja na kuchelewa kuwafikia kwa pembejeo
hizo, bado kuna changamoto ya kutogawiwa kama
inavyotakiwa kwani mara nyingi hawapati mbolea zote, ambapo wakati mwingine
badala ya kupata mifuko mitatu hupata mmoja bila kutolewa maelekezo yoyote.
Naye mkulima Karitas Ndunguru alisema kuwa pamoja na malengo
mazuri ya serikali mara nyingi wanaokwamishwa ni watendaji wa kata na vijiji,
ambapo kwa kushirikiana na kamati za vocha za vijiji au kata, huwaibia wakulima
huku wakimhusisha wakala aliyepewa dhamana ya kusambaza pembejeo.
"Serikali yetu inatujali sisi wakulima na ndio maana iliamua
kutoa pembejeo za ruzuku ili kuwasaidia wakulima wadogo wadogo, lakini sasa
tatizo lipo kwa wale ambao wamepewa dhamana ya kusimamia, ni vyema wakabadilika
vinginevyo wataendelea kutukwamisha", alisema.
Kwa upande wake ofisa mtendaji wa kijiji hicho Bw. Ombeni Mekasi
alisema, tatizo kubwa linalowakabili wakulima ni ukosefu wa fedha za kulipia
pembejeo pale zinapopelekwa na wakala katika maeneo yao, na kwamba baadhi yao
huwauzia wafanyabishara mbolea hizo mara baada ya kukabidhiwa.
"Unajua pamoja na matatizo ya mawakala lakini pia nao
wakulima mara nyingi wamekuwa wakikosa fedha za kulipia pembejeo, kutokana na hilo hujikuta
wakirubuniwa kiurahisi na watu wenye fedha ambapo huwapa fedha kwa ajili ya
kulipia na kumkabidhi huyo aliyewapa hizo mbolea au mbegu", alisema.
Aliwataka wakulima ambao watapata vocha za pembejeo za ruzuku,
kutokubali kurubuniwa na wafanyabiashara au wakulima wenye uwezo badala yake
wahakikishe wanazitumia mbolea hizo kwenye mashamba yao, ili waweze kuzalisha mazao kwa wingi.
No comments:
Post a Comment