Na Steven
Augustino,
Songea.
SERIKALI mkoani Ruvuma imesema, imefikia mwisho wa kuendelea kumvumilia mkandarasi anayejenga barabara kwa kiwango cha lami, kutoka wilaya ya Namtumbo kwenda Tunduru mkoani humo, yenye urefu wa kilometa 192 kwa madai kuwa ameshindwa kazi na ujenzi wake haukidhi viwango vinavyotakiwa.
Mkuu
wa mkoa wa Ruvuma Bw. Said Mwambungu amesema hayo na kuitaja kampuni hiyo kuwa
ni ya Progressive Higleig Jv Contractors.
Kauli
hiyo ya mkuu huyo wa mkoa aliisema wakati alipokuwa akifungua kikao cha Bodi ya barabara
mkoani humo, kilichofanyika leo kwenye ukumbi wa Songea Club mjini Songea.
Bw.
Mwambungu alisema kuwa mradi huo ambao ni kati ya miradi inayotekelezwa kupitia
mradi wa maendeleo wa Mtwara Corridor ulioanza mwaka 2010, na ni moja kati ya mradi
pekee ambao hadi sasa bado haujaonesha maendeleo mazuri katika ujenzi wake hivyo serikali haiwezi kuendelea kuvumilia katika hilo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wabunge injinia Ramo Makani wa jimbo Tunduru Kaskazini na Alhaji Mtutura wa Jimbo la Tunduru Kusini waliwataka wajumbe wa bodi hiyo, kuendelea kuishauri serikali kujielekeza kutafuta mkandarasi mwenye uwezo ili aweze kujenga barabara hiyo na sio kama ubabaishaji uliopo sasa.
Naye
mkuu wa wilaya ya Tunduru Bw. Chande Nalicho katika maelezo yake alimtaka wakala wa barabara(TANROADS) mkoani Ruvuma, kuandaa utaratibu wa
kumbana mkandarasi wa kampuni hiyo,
ikiwemo suala kuhakikisha anaachia kazi na kuyakwamua
magari yanayokwama kipindi hiki cha masika kutokana na barabara kukwanguliwa na
kuwekwa kifusi ambacho kinasababisha tope na kusababisha magari kukwama na kuwa kero kwa abiria wanaotumia barabara hiyo.
Bw.
Nalicho aliendelea kufafanua kuwa hali hiyo inatokana na kampuni hiyo kuzembea kutimiza majukumu iliyopewa na serikali ya kujenga barabara hiyo, kuiharibu barabara kutokana
na kuondoa sehemu ya juu ya udongo wa changarawe ambayo ilikuwa tokea awali.
No comments:
Post a Comment