Hili ni jengo la kisasa la kuhifadhia maiti katika hospitali ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Ujenzi wake bado unaendelea na sasa limefikia hatua ya mwisho katika kumaliza ujenzi huo. (Picha na Kassian Nyandindi)
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
SERIKALI nchini kupitia wizara yake
ya afya imejenga jengo la kisasa la kuhifadhia maiti katika hospitali ya wilaya
ya Mbinga mkoani Ruvuma, ikiwa ni lengo la kuondokana na adha ya muda mrefu,
iliyokuwa ikiikabili hospitali hiyo sehemu maalum ya kuhifadhi maiti ili
zisiweze kuharibika.
Taarifa za uhakika zinasema kwamba ujenzi
huo utagharimu shilingi milioni 145 ambapo hivi sasa kazi ya ujenzi imefikia
hatua za mwisho kukamilisha jengo hilo.
Mradi huo unajengwa kwa kufuata
michoro maalum iliyoelekezwa na wizara ya afya kupitia wataalamu wake.
Licha ya ujenzi wake kugharimu muda
wa miezi minne, mpaka sasa tokea lianze kujengwa mapema mwanzoni mwa mwaka huu, muda huo umepita na bado
halijakabidhiwa rasmi jambo ambalo linazua maswali mengi miongoni mwa jamii.
Hospitali hiyo ina zaidi ya miaka 25
mpaka sasa tokea ianzishwe haikuwa na jengo la kisasa la kuhifadhia maiti,
badala yake maiti zilikuwa zikihifadhiwa kienyeji kutokana na kukosa vyombo
maalum vya kuhifadhia.
Kadhalika jengo hilo la kuhifadhia
maiti ambalo linajengwa katika hospitali ya wilaya ya Mbinga, litakuwa na uwezo
wa kuhifadhi maiti 84 kwa siku katika mafriji ya kisasa yatakayohifadhiwa hapo.
“Mara baada ya kukamilika kwa ujenzi
wa jengo hili mtaalamu husika ataweka mafriji ya kisasa ndani ya jengo, ambayo
yataweza kutunza na kuhifadhi maiti zisiharibike”, kilisema chanzo chetu
ambacho kiliomba jina lake lisitajwe.
No comments:
Post a Comment