Mahindi yakiwa yameoteshwa shambani kwa kufuata kanuni bora za kilimo.
Na Dustan Ndunguru,
Mbinga.
WAKULIMA 34,752 wilayani
Mbinga mkoa wa Ruvuma watanufaika na pembejeo za ruzuku katika msimu wa kilimo
wa mwaka 2012/2013 ikiwa ni pungufu ikilinganishwa na wakulima 46,517 waliopata
pembejeo hizo msimu uliopita.
Akiongea na mwandishi wa
habari hizi ofisini kwake ofisa kilimo na ushirika wa wilaya hiyo Bw. Yonas
Nyoni alisema msimu wa mwaka 2011 hadi 2012 jumla ya vocha 139,551 zilipokelewa
ikilinganishwa na msimu huu wa mwaka 2012 hadi 2013 ambapo jumla ya vocha
104,256 zinatarajiwa kupokelewa.
Bw. Nyoni alisema kuwa
katika msimu huu wa kilimo mahitaji halisi ya mbolea ni tani 28,652.60 na
mahitaji ya mbegu ni tani 398 na kwamba alizitaja mbegu hizo kuwa ni za mahindi
aina ya chotara tani 350, mahindi 0PV tani 45 na mpunga tani 3.
Alisema mbolea aina ya urea
zinahitajika tani 9,550.90,minjingu tani 9,550.90 DAP tani 4,775.40 na S/A tani
4,775.40 na kwamba tayari makampuni yaliyopewa kazi ya kusambaza pembejeo hizo
kwa wakulima yamekwisha anza kazi ya kuleta wilayani humo.
Alieleza kuwa idara ya
kilimo wilayani humo ilikwishawaelekeza wakulima juu ya umuhimu wa kujiwekea
akiba ya kutosha, ili kwa mkulima ambaye hatapata pembejeo za ruzuku aweze
kununua pembejeo kutoka kwenye maduka ya wafanyabiashara binafsi kwa ajili ya kuboresha
mazao yaliyomo shambani.
Kadhalika kwa wale
watakaobahatika kupata pembejeo za ruzuku wazitumie kwa malengo yaliyokusudiwa.
Vilevile aliyataka
makampuni kumi ambayo yamepewa kazi ya kusambaza pembejeo hizo kwa wakulima,
kuhakikisha kwamba yanatekeleza majukumu yao ipasavyo na kwa wakati ili wakulima
waweze kuzitumia na hivyo kuwawezesha wazalishe mazao mengi na yaliyo bora.
Alisema kuwa serikali
mwaka huu imeamua kuanzisha mfumo mpya wa usambazaji wa mbolea ambapo makampuni
ndiyo yaliyopewa dhamana ya kusambaza kwa wakulima, na kwamba makampuni hayo
nayo yataandaa mawakala wao ambao watazifikisha pembejeo hizo kwa mkulima
husika.
Pia ofisa kilimo huyo
aliwataka maofisa ugani wilayani Mbinga kuhakikisha katika ngazi za kata na
vijiji, kuhakikisha wanatoa elimu kwa wakulima ili hatimaye waweze kuzalisha
kwa kutumia utaalamu na kwamba wakulima nao, kwa upande wao wazingatie
maelekezo yanayotolewa na wataalamu kupitia mashamba darasa yaliyopo.
No comments:
Post a Comment