Saturday, November 10, 2012

MBUNDA: JENGENI USHIRIKIANO KATIKA CHAMA



Mwenyekiti wa chama cha mapinduzi (CCM) wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma Bw. Christantus Mbunda, alipokuwa akizungumza na mwandishi wa habari hizi makao makuu ya ofisi za chama hicho wilayani humo hivi karibuni. 




 

Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

CHAMA cha mapinduzi(CCM) wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, kimewataka wanachama wake kuhakikisha kwamba wanajenga ushirikiano katika kutekeleza ilani ya chama hicho ili kuleta imani kwa wananchi waliokiweka madarakani.

Mwenyekiti wa CCM wilayani humo Bw. Christantus Mbunda alisema hayo wakati alipokuwa akizungumza na mwandishi wa habari hizi katika ofisi za makao makuu ya chama hicho wilayani Mbinga.

Bw. Mbunda alisema, itakuwa ni jambo la kushangaza kuona viongozi au makada wa chama hicho kuanza kujenga matabaka ya kukigawa chama, hali ambayo itawafanya wapinzani wapate mwanya wa kukipaka matope.

Alisema ni wakati muafaka sasa wa viongozi wa chama hicho wilayani humo, kukaa chini na kupanga mikakati ya kuboresha miradi ya chama iliyopo sasa, ikiwemo kuwatafuta wawekezaji ili iweze kuwa endelevu na kukiingizia chama mapato.

”Huu ni wakati muafaka sasa kila mmoja wetu kuwajibika katika eneo lake, si wakati wa kukaa vijiweni na kuanza kupika majungu ambayo hayataweza kutusaidia katika kufikia malengo yetu”, alisema.

Hata hivyo aliongeza kuwa uongozi wa chama hicho umeweka mikakati ya kupita katika kila kata za wilaya ya Mbinga, na kuelezea maendeleo yaliyofanywa na chama cha mapinduzi ili wananchi waweze kutambua na kuelewa.

No comments: