Katibu mwenezi wa chama cha
mapinduzi mkoani Ruvuma Bw. Benedict Ngwenya akizungumza na vyombo mbalimbali vya habari leo mkoani humo(hawapo
pichani) katika ofisi za chama hicho mjini Songea, kulia ni katibu wa umoja wa vijana (UVCCM) wa mkoa Bi. Mwajuma
Rashid na kushoto Mwenyekiti CCM mkoani Ruvuma Bw. Oddo Mwisho.
Na Dustan Ndunguru,
Songea.
MWENYEKITI
wa chama cha mapinduzi(CCM) mkoa wa Ruvuma Bw. Oddo Mwisho amesema, mwanachama
wa chama hicho ambaye ataendekeza makundi kwa lengo la kukigawa chama na
wanachama kwa ujumla, atachukuliwa hatua kali kulingana na taratibu za chama
ikiwemo kukalishwa kitako katika vikao halali.
Bw.
Mwisho alisema kinachotakiwa sasa ni wanachama wenyewe kuwa na maadili mema na
sio kuendeleza malumbano yasiyokuwa ya msingi.
Hayo
alisema wakati alipokuwa akizungumza na vyombo mbalimbali vya habari mjini
Songea, huku akifafanua kwamba hivi sasa
chama hicho kimekuwa kikiwaelekeza wanachama wake kote nchini juu ya umuhimu wa
kuyaondoa makundi yaliyotokana na uchaguzi kwa malengo ya kukijenga chama.
“Makundi
katika chaguzi mbalimbali za chama lazima yawepo, kila kundi linakuwa na
mgombea wake ambaye linamuunga mkono hivyo kinachotakiwa mara baada ya
kukamilika kwa uchaguzi na viongozi kupatikana, linatakiwa libaki kundi moja tu ambalo
linakijenga chama kwa mazuri”, alisema.
Hata
hivyo alieleza kuwa hatarajii makundi kuendelea kuwepo mkoani Ruvuma,
badala yake anaimani mshikamano taendelea kudumu wakati wote.
Kadhalika
aliongeza kuwa baada ya kukamilika kwa chaguzi mbalimbali za chama, hivi sasa
wanajipanga kushinda chaguzi zijazo za serikali, ambapo kwa kuanzia
wanayomatarajio makubwa ya kuibuka na ushindi mkubwa katika uchaguzi wa
serikali za mitaa, hivyo mafanikio hayo yatafikiwa pakiwa hakuna makundi
yanayosigana ndani ya chama.
Aidha
Bw. Mwisho alisema moja ya mkakati ambao wamejiwekea kwa sasa ni kuhakikisha
wanaanzisha madarasa ya itikadi, ambayo yatatumika kuwapa elimu ya siasa
wanachama wake kabla hawajakubaliwa kujiunga kama
wanachama na kwamba mkoa huo unao makada wengi ambao watawatumia kwenda kwenye
mashina, tawi na kata kutoa elimu hiyo.
"Hapo
awali kulikuwa na madarasa hayo ambayo kimsingi yalikuwa msaada mkubwa kwa
chama chetu, hapa kwetu tumeamua kwa dhati kuyarudisha kwani yatatoa mwongozo
kwa wanachama wetu watakaoomba kujiunga na chama chetu", alisema Bw. Mwisho.
Pamoja
na mambo mengine aliwashukuru wananchi wa kata za Mpepai wilayani Mbinga na
Mletele wilaya ya Songea, kwa kuwachagua wagombea wa chama hicho katika
uchaguzi mdogo wa udiwani uliofanyika Oktoba 28 mwaka huu.
No comments:
Post a Comment