Rais Jakaya Kikwete |
Na Dustan Ndunguru,
Songea.
CHAMA cha mapinduzi (CCM) mkoani Ruvuma kimesema, kuibuka
kwa ushindi wa kishindo katika chaguzi ndogo kwa nafasi za udiwani
uliofanyika Oktoba 28 mwaka huu, ni ushahidi tosha kuwa chama hicho
kinakubalika tofauti na madai yanayotolewa na wapinzani ambao wamekuwa wakidai hakina mvuto kwa watanzania.
Katibu wa CCM wa mkoa huo Bi. Verena
Shumbusho alisema kuwa katika uchaguzi huo ambao ulifanyika katika kata
za Mletele manispaa ya Songea na kata ya Mpepai iliyopo wilayani
Mbinga, wananchi waliwachagua wagombea wa chama hicho kwa kura nyingi
baada ya kuridhishwa na sera nzuri sambamba na utekelezaji wa yale
ambayo waliahidiwa mwaka 2010.
Bi. Verena alisema kuwa ushindi huo ni mwanzo mzuri kwa chama
hicho, hasa katika kipindi hiki cha kuelekea katika chaguzi za serikali
za mitaa na uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 ambapo kinachotakiwa kwa sasa ni
kwa viongozi na wanachama kujipanga vizuri huku wakitakiwa kukanusha
taarifa zinazotolewa na wapinzani dhidi ya CCM zenye kulenga
kukidhoofisha.
Alisema kuwa wakati wote wa kampeni vyama vya upinzani
vilikuwa vikitoa maneno mabaya ambayo yalilenga kukidhoofisha chama cha
mapinduzi, lakini mwisho wa siku wananchi walifanya maamuzi sahihi
yatakayopelekea wasonge mbele kimaendeleo kama walivyoahidiwa katika
mikutano ya kampeni ya chama hicho.
"Chama chetu kilipitia mabonde na milima katika uchaguzi
huo mdogo lakini imani waliyonayo wananchi kwetu waliwachagua wagombea
wetu tena kwa kura nyingi, tofauti na dhamira waliyokuwa nayo hawa
wenzetu", alisema.
Katibu huyo aliwashukuru wanachama, wapenzi na wananchi kwa
ujumla kutokana na ushindi huo ambapo alisema kuwa kilichobaki kwa sasa
ni kwa madiwani waliochaguliwa kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao
ipasavyo ili wananchi waweze kujenga imani kwao na kwa chama cha
mapinduzi.
Alisema baada ya kukamilika kwa uchaguzi huo mshikamano
unapaswa kuwepo baina yao kwa malengo ya kufanikisha utekelezaji wa
ilani ya uchaguzi ya mwaka 2010 na kwamba viongozi wa vyama vya upinzani
wahakikishe wanahamasisha wafuasi wao kujitokeza kuchangia nguvu zao
kwenye utekelezaji wa miradi ya kimaendeleo.
"Hata kama wagombea wao hawakuchaguliwa ningewaomba hawa
wenzetu wahamasishe wafuasi wao wajitokeze kuchangia nguvu zao katika
ujenzi wa miradi pale wanapohitajika kwa sababu watakaonufaika nayo sio
wana CCM pekee bali ni wote kwani ilani ya CCM haina ubaguzi", alisema Bi.
Verena.
No comments:
Post a Comment