Na
Dustan Ndunguru,
Tunduru.
MAHAKAMA
ya wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma imemhukumu
mkazi mmoja wa kijiji cha Nalasi wilayani humo, adhabu ya kifungo cha miaka 30
kwenda jela pamoja na kuchapwa viboko 10 kwa kosa la ubakaji.
Akisoma
hukumu hiyo hakimu mkazi katika mahakama ya wilaya hiyo Bw. Ernest Mgongolo
alisema, mahakama hiyo imeridhika na ushahidi uliotolewa na upande wa mashitaka
kuwa mshitakiwa Issa Mwichande(27) alimbaka mwanafunzi mwenye miaka 11 wa shule
ya msingi Nalasi.
Bw.
Mgongolo alisema kuwa mahakama imemtia hatiani na kuhukumiwa adhabu ya kifungo
cha miaka 30 kwenda jela, sambamba na kuchapwa viboko kumi ambapo viboko vitano
atachapwa wakati wa kuingia na vitano wakati wa kutoka akishamaliza kutumikia
kifungo hicho.
Awali
mwendesha mashitaka wa polisi Inspekta Minde alidai mahakamani hapo kuwa,
mshitakiwa huyo alitenda kosa hilo
Oktoba mwaka jana saa za asubuhi nyumbani kwa mwanafunzi huyo.
Wakati
huo huo mkazi mmoja wa kijiji cha Lukumbule wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, amehukumiwa na mahakama ya wilaya hiyo, adhabu ya
kifungo cha miaka 3 kwenda jela baada ya kupatikana na kosa la kumbaka
mwanafunzi wa darasa la saba.
Akisoma
hukumu hiyo Hakimu mkazi katika mahakama ya wilaya ya Tunduru Bw. Ernest
Mgongolo alisema kuwa mahakama, imeridhika na ushahidi uliotolewa na upande wa
mashitaka kuwa mshitakiwa Bakari Ismail Bakari(20) alimbaka mwanafunzi wa
darasa la saba shule ya msingi Lukumbule.
Hakimu
huyo alisema kuwa mahakama imemtia hatiani na kumhukumu adhabu ya kifungo cha
miaka mitatu kwenda jela, viboko vitano, faini ya shilingi milioni 3 na kulipa
fidia ya shilingi milioni moja.
Awali
mwendesha mashitaka wa polisi Inspekta Minde alidai mahakamani hapo kuwa,
mshitakiwa Bakari alitenda kosa hilo mwezi Oktoba mwaka huu, saa za asubuhi
wakati mwanafunzi huyo akiwa nyumbani kwake Lukumbule.
No comments:
Post a Comment