Na
Kassian Nyandindi,
Mbinga.
BENKI
ya NMB tawi la Mbinga mkoa wa Ruvuma
imesitisha huduma ya kuuliza salio, kununua na kutoa salio kwa njia ya simu kwa
mtandao wa (AIRTEL MONEY) kupitia benki hiyo kwa baadhi ya wateja wake, ambao wametoa malalamiko, kwa
kile kinachodaiwa kwamba mfumo huo umeingiliwa na matapeli ambao wanaiba fedha
za wateja waliojiunga nao, kupitia akaunti zao ambazo wamezifungua katika benki
hiyo.
Utafiti
uliofanywa na mwandishi wa habari hizi kwa nyakati tofauti umebaini kuwa,
wateja walioibiwa fedha zao na ambao wamelalamika kutapeliwa kupitia mfumo huo,
ni baadhi ya wafanyakazi wa halmashauri ya wilaya hiyo na wananchi wa kawaida.
Mwandishi
wa habari hizi ameshuhudia hata mawakala wa mtandao wa airtel waliopo Mbinga
mjini, wakisumbuliwa na wateja wao wakidai kwamba kuna watu kuanzia Alhamisi ya
tarehe 25 Oktoba mkwaka huu mpaka sasa, walikuwa wakipigiwa simu na watu
wanaojitambulisha kutoka makao makuu ya mtandao huo, kwamba wanatakiwa watoe
baadhi ya taarifa za usajili wa laini zao za simu kwa kile walichoambiwa
kwamba majina yao yamechaguliwa kwa ajili ya kuyashindanisha kwenye
promosheni(michezo ya bahati nasibu) na baadaye wakishinda waweze kupata zawadi.
Akizungumza
kwa sharti la kutotajwa jina lake, mmoja kati ya waathirika wa tukio hilo(ambaye ni mteja wa airtel) alisema yeye alipopigiwa
simu hiyo aliambiwa kama ifuatavyo;
Namnukuu:
“Kwanza
nilipigiwa simu na mtu ambaye alijitambulisha jina ambalo kwa sasa silikumbuki
akisema, unaongea na makao makuu ya airtel, jioni hii tunafanya promosheni
nyingine kama zile zilizopita kipindi cha
nyuma katika mkoa wako”,
“Mshindi
wa kwanza atapata milioni 30, wa pili 20 na watatu milioni 10, wewe ni mmoja
kati ya watano walioteuliwa lakini watakaoshindanishwa katika promosheni hii ni
majina matatu tu kati ya hayo matano”,
“Hivyo
tunaomba ututajie kwanza huduma unazozitumia katika mtandao wa airtel, majina
yako matatu, namba yako ya simu, mwaka uliozaliwa, mkoa uliopo, mtaa unaoishi
na akaunti namba ya benki”.
Anasema
baada ya kutaja vitu hivyo na maswali mengine mengi ambayo alikuwa akiulizwa,
baada ya kumaliza maongezi tu na “tapeli huyo” aliyempigia, utakuta simu
inakatwa mawasiliano na laini haifanyi kazi tena.
Anaeleza
kwamba baada ya siku moja kupita alipokwenda benki alikuta salio lake limehamishwa,
ndipo alipotoa taarifa kwa uongozi husika wa benki na kuchukua maamuzi ya
kujaza fomu maalum kwa ajili ya tatizo lake kufanyiwa
kazi.
Wateja
ambao walijiunga na huduma hiyo ya mtandao wa airtel ambao baadhi yao wamefanyiwa hujuma kama
hiyo, wamesitisha huduma ya airtel money katika benki ya NMB kupitia tawi la
Mbinga, ambao taarifa zao zimeripotiwa katika benki hiyo na kujaza fomu maalum
kwa ajili ya kufanyiwa kazi.
Hivi
sasa tunayo majina ya watu watano ambao wamejaza fomu hizo(majina na namba zao
za simu tunayo) baada ya kufanyiwa hujuma hizo.
Kwa
mujibu wa chanzo cha uhakika kutoka NMB kimedai kuwa tatizo hilo
limekuwa likijitokeza maeneo mengi na wao sio mara yao
ya kwanza kulisikia au kuletewa malalamiko kama
haya, huku ikidaiwa kuwa linafanywa na wafanyakazi wa airtel ambao sio
waaminifu.
“Wengine
ambao wana namba zetu za simu hapa ofisini waliwahi kutupigia na kutuomba
tuzuie akaunti zao baada ya kupigiwa simu na watu wanaodaiwa ni wa kutoka makao
makuu ya airtel, sisi tukazuia akaunti zisifanye kazi kwa muda ili wasiweze
kuibiwa,
“Lakini
kwa wale waliochelewa, ndio kama hivi wameibiwa na tunawashauri hata kama kuna watu wanapigiwa simu za mtindo huu wazipuuze,
wasiendelee kuongea nazo na kutoa taarifa za huduma zao za fedha za mtandao wa
simu”, kilisema chanzo hicho.
Mwandishi
wa habari hizi alipofanya mahojiano na Meneja wa mawasiliano wa airtel makao
makuu Dar es Salaam,
aliyejitambulisha kwa jina la Jackson Mbando(0786670120) alisema kampuni ya
airtel hivi sasa haiendeshi mashindano ya promosheni.
Alisema
utoaji na uwekaji wa pesa kwenye akaunti za wateja wa mtandao wa kampuni hiyo,
endapo kuna tokea matatizo kama haya ni uzembe
unaofanywa na wateja katika kutoa taarifa zao ikiwemo “Password”, hivyo wateja
wanatakiwa kuwa makini kutotoa taarifa hizo ili wasiibiwe fedha zao.
Alisema
kwa wale waliofanyiwa hivyo waende kuripoti kituo cha polisi, “Kitu kama hiki
hakikuwa na sababu ya kuendelea kukijadili ni vyema nashauri waende polisi na
taratibu za kisheria ziweze kuendelea”, alisema Bw. Mbando.
Pamoja
na majibu hayo bado mwandishi wetu aliendelea kufanya mawasiliano kwa njia ya simu
na Mkurugenzi wa Mawasiliano wa kampuni ya airtel makao makuu Dar es salaam, naye
alijitambulisha cheo hicho na jina lake, Beatrice Singano(0784670277) ambapo
alipoulizwa juu ya hujuma hizo walizofanyiwa wateja wake hapa Mbinga, mkoani Ruvuma alisema,
“Sisi
kampuni yetu haina taarifa juu ya tukio hili, na vilevile hatuendeshi
promosheni, nasema sina taarifa ndio kwanza nimeipata kutoka kwako”, alisema.
Kadhalika
aliongeza kuwa endapo taarifa hiyo itawafikia rasmi ofisini kwao, “Tupo tayari
kutoa ushirikiano wa aina yoyote katika hili, mara tupatapo taarifa kamili,
hivi sasa kwa kweli hatuna taarifa kamili juu ya tukio hili”, alisisitiza.
No comments:
Post a Comment