Baadhi ya wazee wa wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, wakimsikiliza mkuu wa wilaya hiyo Bw. Chande Nalicho katika kijiji cha Chiwana wakati wa kilele cha wiki ya elimu ya watu wazima wilayani humo.
Na Dustan
Ndunguru,
Tunduru.
WANAFUNZI 2436 waliopangwa kuanza kidato cha kwanza wilayani
Tunduru mkoani Ruvuma, baada ya kuhitimu darasa la saba mwaka jana hawajaripoti
katika shule walizopangiwa kwenda kusoma, ambapo wanafunzi 1603 sawa na
asilimia 35 ndio walioripoti shuleni kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo
utoro na mimba.
Akifungua
kikao cha baraza la madiwani kilichofanyika hivi karibuni katika ukumbi wa
mikutano wa halmashauri mjini hapa mwenyekiti wa halmashauri hiyo Bw. Faridu
Hamis alisema wanaopaswa kulaumiwa hasa ni wazazi, ambapo pamoja na kuwepo kwa
jitihada za makusudi za kuhamasisha watoto wanaofaulu mitihani yao ya darasa la
saba waendelee na masomo bado jitihada hizo hazileti mafanikio.
Bw. Hamis alisema tatizo hilo sugu la wazazi
kutowapeleka shule watoto wao ambao wamefaulu kuendelea na masomo ya sekondari,
sasa limekuwa la kawaida kwa wazazi na walezi wa watoto hao na kwamba wakati
umefika kuwachukulia hatua za kisheria ukizingatia kwamba huu si wakati wa
kubembelezana katika masuala ya erlimu.
"Hebu
waheshimiwa madiwani fikirieni hadi kufikia Julai mwaka huu kati ya watoto 2436
waliopangwa kuanza kidato cha kwanza, ni wanafunzi 1603 tu sawa na
asilimia 35 ndio walioripoti mashuleni, jamani tunaenda wapi kwa kweli hili ni
tatizo kubwa", alisema.
Alisema
wilaya hiyo bado inakabiliwa na changamoto kubwa ya kuhamasisha wazazi wafahamu
umuhimu wa elimu, ili watoto wao wanapofaulu kuwaendeleza kimasomo jambo ambalo
litasaidia wapate uelewa na hatimaye kuwa na ujasiri wa kuendesha maisha yao
kwa umakini mara watakapohitimu masomo yao.
Alieleza zaidi kuwa katika
wanafunzi 883 ambao hawajaripoti wapo ambao wamepata mimba tatizo
ambalo ni sugu katika halmashauri hiyo, kwani wazazi wa watoto hao wamekuwa
wakiwaficha waliofanya uhalifu huo na kukwamisha juhudi za serikali za
kuhakikisha watoto wa kike, nao wanapata elimu sawa na ilivyo kwa watoto wa
kiume.
Mwenyekiti
huyo wa halmashauri alisema kuwa hivi sasa tayari msako mkali wa kuwatafuta
wanafunzi ambao hawajaripoti katika shule walizopangiwa umeanza, hivyo wazazi
wao ambao hawajawapeleka watoto wao shule watawafikisha mahakamani ili iwe
fundisho kwa watu wengine ambao watafanya vitendo hivyo.
No comments:
Post a Comment