Friday, November 23, 2012

WAKAZI TUNDURU MJINI AFYA ZAO ZIPO HATARINI, WANANCHI WAULALAMIKIA UONGOZI WA WILAYA

Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Bw. Said Mwambungu.
















Na Steven Augustino, 
Tunduru.

ABIRIA na Wananchi wanaotumia Kituo kikuu cha mabasi  mjini Tunduru mkoani Ruvuma, wamelalamikia kuendelea kukithiri kwa uchafu katika kituo hicho na kuhofia usalama wa afya zao.

Waandishi wa habari ambao wamezungumza na abiria na baadhi ya wananchi kwa nyakati tofauti, kwa masharti ya kutotajwa majina yao, walisema mbali na kuwepo kwa utaratibu wa halmashauri ya wilaya hiyo, kutoza ushuru wa aina mbalimbali ikiwemo magari yanayoegeshwa katika kituo hicho hali bado ni tete na hakuna juhudi zozote
zinazoonyesha kuzaa matunda katika kukabiliana na suala hilo.

Walisema ushuru ambao hutozwa ni shilingi 1000 kwa kila gari linaloingia na kutoka katika kituo hicho, na magari  yanayoegeshwa ndani ya kituo hicho hutozwa shilingi 1000 kwa kila gari linalo egeshwa hadi asubuhi.

Imeelezwa kwamba adha wanazozipata kutokana na uchafu huo kuzagaa ovyo katika maeneo mbalimbali ya kituo, wamekuwa wakikerwa na harufu kali zinazotokana na kuwepo kwa vinyesi na mikojo katika miwambaza  ya kituo hicho, jambo ambalo ni hatari kwa afya ya binadamu.

“watumishi wa idara ya afya wameutelekeza mji huu, hata maeneo mengine ukipita utakuta ni kuchafu, kikiwemo na kituo hiki cha mabasi”, walisema.

Kingine kinacho wa kwaza abiria hao na wakazi wa Tunduru mjini, ni pamoja na kushamiri kwa uchafu katika vyoo ambavyo hutumiwa na abiria na wananchi hao na maeneo mbali mbali ya biashara, ikiwemo migahawa na mabaa yameonekana kuendelea kukithiri kwa uchafu.

Jitihada za kumpata afisa afya wa halmashauri ya wilaya hiyo aliyefahamika kwa jina moja Mhagama ziligonga mwamba, baada ya simu yake ikipigwa kuita muda mrefu, bila kupokelewa hadi habari hizi zinaingia mitamboni.

Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Tunduru Bw. Robert Nehatta mbali na kukiri kukithiri kwa uchafu katika mji wake wa wilaya hiyo, alisema kuwa chanzo cha uchafu huo kinatokana na kukosekana kwa mafuta ambayo yangetumika katika magari ya kubebea takataka hizo na kuzimwaga katika eneo maalum linalotumika kuziteketeza.

Uchunguzi umebaini kuwa mafuta ni tatizo la kudumu katika mji huo, na halmashauri hiyo haina magari ya kubebea taka muda mrefu sasa, ambapo inategemea kubeba taka hizo kwa kutumia trekta moja ambalo ni chakavu.

No comments: