Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
HUENDA maafa makubwa yatajitokeza katika shule ya Msingi
Myangayanga, iliyopo kijiji cha Myangayanga Wilaya ya Mbinga mkoani
Ruvuma , kutokana na jengo moja linalotumika kusomea wanafunzi kuwa
katika hali mbaya.
Mwandishi
wa habari hizi ambaye alitembelea shule hiyo ameshuhudia jengo hilo
lilivyokuwa, ambapo ni chakavu na limekuwa na nyufa kubwa huku watoto na
walimu wa shule hiyo wakiendelea kulitumia wakati wa vipindi vya
masomo.
Jengo
hilo ambalo lina vyumba vinne limekuwa likitumika kusomea wanafunzi wa
darasa la awali, darasa la tatu na la nne na kwamba lina ofisi tatu za
walimu hivyo huenda likabomoka wakati wowote.
Mwalimu
mkuu wa shule hiyo Bw. Maxensius Kiyao ameliambia gazeti hili kwamba
jumla ya wanafunzi 140 na walimu sita wakati wa masomo kwa siku
hulitumia jengo hilo kutokana na upungufu wa vyumba vya kusomea, jambo
ambalo ni hatari kwao.
Alisema
jitihada za kulikarabati zimegonga mwamba kutokana na kukosa fedha,
hivyo uongozi husika wa halmashauri ya kijiji cha Myangayanga na wa
wilaya ya Mbinga, unapaswa kuchukua hatua za makusudi katika kunusuru
hali hiyo ili lisiweze kuleta madhara makubwa baadaye.
Bw.
Kiyao alisema tatizo hili ni la muda mrefu lina zaidi ya miaka miwili
sasa iliyopita na taarifa katika ngazi za juu halmashauri ya wilaya hiyo
zimekwisha pelekwa lakini utekelezaji hakuna.
“Jengo
hili kama unavyoliona limechakaa na lina nyufa kubwa jambo ambalo ni
hatari na linatishia amani kwa watoto wetu, linahitaji nguvu kubwa
katika kulikarabati”, alisema.
Alifafanua
kwamba uongozi husika wa halmashauri ya wilaya ya Mbinga baada ya
kupewa taarifa juu ya hali mbaya ya jengo hilo , ulituma wataalamu
kutoka idara ya ujenzi ambao walikwenda kufanya upembuzi yakinifu juu ya
tatizo hilo .
Alisema
tokea wataalamu hao wamekwenda kufanya kazi hiyo ni miaka miwili sasa
imepita hakuna jitihada zilizozaa matunda na jengo linaendelea kuwa
katika hali mbaya.
Kadhalika
aliongeza kuwa shule hiyo inakabiliwa na tatizo la nyumba za walimu
wengi wao hupanga uswahilini ambapo zilizopo ni tatu tu.
Wakizungumza
kwa nyakati tofauti wakazi wa kijiji hicho walisema hata Mbunge wao wa
Mbinga Mashariki Bw. Gaudence Kayombo wakati wa kampeni za uchaguzi
uliopita mwaka 2010, walimweleza juu ya tatizo hilo na kuwaahidi kwamba
atachangia nguvu zake kwa kuwanunulia vifaa vya viwandani wakati
ukarabati utakapoanza.
Walisema
tokea Mbunge huyo atoe ahadi hiyo ya kuwachangia hawajawahi kumuona
tena kijijini hapo na hakuna taarifa zozote zinazoonesha jitihada za
kumaliza kero hiyo na wananchi wapo tayari kuchangia nguvu zao kama vile
tofari, mchanga na mbao.
“Huyu
Mbunge tumemuona hapa wakati wa kampeni tu, tokea amepata madaraka
hajawahi hata kututembelea hapa kijijini, alisema Alfrida Komba.
Mbunge
Kayombo alipoulizwa juu ya suala hilo alisema yeye hajawahi kutoa ahadi
yoyote kwa wananchi hao ya kuchangia ukarabati wa jengo hilo .
“Hapana
sijawahi kutoa ahadi ya mchango wowote katika kulikarabati jengo hilo ,
ila nakumbuka mtaalamu wa ujenzi tulimtaka aende kule ili aliangalie na
kutuletea majibu kama jengo linafaa kukarabatiwa au kulibomoa lote na
kujenga upya”, alisema.
Kwa
ujumla shule ya msingi Myangayanga ina jumla ya wanafunzi 391 kutoka
darasa la awali mpaka darasa la saba hivyo jitihada za kuboresha
mazingira ya shule hiyo zinahitajika kutekelezwa mapema kabla ya
kujitokeza matatizo makubwa baadaye.
Alipotakiwa
kutoa ufafanuzi juu ya hali hiyo ofisa elimu shule za Msingi Wilaya ya
Mbinga Bw. Mathias Mkali alisema taarifa juu ya ubovu wa jengo hilo
ofisi yake haina taarifa, ambapo alisema atafanya utaratibu wa
kufuatilia tatizo hili.
Bw.
Mathias alisema hivi sasa utaratibu wa kujenga miundombinu ya shule
ikiwemo majengo ya shule na nyumba za walimu ni jukumu la halmashauri ya
kijiji husika kwa kushirikisha wananchi kuchangia nguvu zao na serikali
kuwasaidia vifaa vya viwandani.
Akizungumzia
suala la upungufu wa nyumba za walimu alisema wilaya hiyo imekuwa na
matatizo makubwa ya upungufu wa nyumba za walimu na kwamba zilizopo sasa
nyingi ni chakavu.
No comments:
Post a Comment