Baadhi ya Wahariri na Waandishi wa habari wakiwa kwenye mkutano na TFDA katika ukumbi wa hospitali ya mkoa wa Mbeya. |
Mkurugenzi wa huduma za maabara kutoka Mamlaka ya chakula na dawa (TFDA) Charys Ugullum,(aliyesimama) akizungumza na Wahariri na Waandishi wa habari Jijini Mbeya wakati wa ufunguzi wa mkutano huo. |
Baadhi ya Waandishi wa habari na Wahariri wa Nyanda za juu Kusini, wakiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa Mamlaka ya chakula na dawa (TFDA). (Picha zote na Kassian Nyandindi) |
Na Kassian Nyandindi,
Mbeya.
HALMASHAURI za wilaya hapa nchini kupitia kamati zake za udhibiti
wa ubora wa chakula na dawa, zimetakiwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo ili
kuweza kulinda afya za wananchi.
Rai hiyo ilitolewa na Mkurugenzi wa huduma za maabara kutoka
Mamlaka ya chakula na dawa Tanzania (TFDA) Charys Ugullum alipokuwa akizungumza kwenye
mkutano wa siku moja, Wahariri na Waandishi wa habari wa mikoa ya Nyanda za juu
Kusini Jijini Mbeya.
Mkutano huo ulifanyika katika ukumbi wa Hospitali ya mkoa huo,
ambapo ulilenga kuwaelimisha Wahariri na Waandishi wa habari namna ya kuibua matatizo ya bidhaa feki ambazo
huuzwa maeneo mbalimbali hapa nchini, kwa lengo la kuleta ufanisi na ubora wa
chakula na dawa.
“Niwaombe ndugu zangu kwa kutumia wadau kama ninyi tutaweza
kudhibiti ubora wa dawa zetu, fanyeni uchunguzi maduka mengi yamekuwa yakiuza
bidhaa ambazo hazijasajiliwa na ni hatari kwa afya zetu”, alisema Ugullum.
Naye Mkurugenzi wa kitengo cha uendeshaji huduma kutoka TFDA udhibiti
wa vyakula, dawa, vipodozi na vifaa tiba Chrispin Severe alisema kumekuwa na tatizo
la wafanyabiashara wengi, ambao sio waaminifu wamekuwa wakiuza bidhaa hizo ambazo
hazifai kwa matumizi ya binadamu.
Alisema Mamlaka hiyo itaendelea kuteketeza kila bidhaa ambayo
itaona haifai kwa matumizi ya binadamu, ambapo alieleza kuwa tatizo la bidhaa
duni na bandia Nyanda za juu kusini limekuwa kubwa.
“Tutaendelea kuteketeza na kuchukua hatua za kisheria pale
tunapobaini sehemu fulani kuna tatizo, na ndio maana leo tumeamua
kuwashirikisha waandishi wa habari ili muweze kutoa matangazo juu ya mambo haya”,
alisema.
Pamoja na mambo mengine mkutano huo ambao ulikuwa wa siku
moja, TFDA ilikutana na Wahariri na Waandishi wa habari wa Nyanda za juu kusini
kutoka mikoa ya Mbeya, Iringa, Njombe, Rukwa na Katavi.
No comments:
Post a Comment