Askofu Mkuu wa Jimbo kuu la Songea mkoani Ruvuma, Damian Dallu. |
Na Kassian Nyandindi,
Songea.
ASKOFU mkuu wa Jimbo kuu la Songea mkoani Ruvuma,
Mhashamu Damian Dallu amewataka Watanzania kuuenzi na kudumisha Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ambao umedumu kwa miaka 50 sasa, kwa
manufaa ya wananchi wa pande zote mbili.
Pia alisema Watanzania waliungana kwa moyo wao wenyewe
na sio kwa karatasi, hivyo wanaohangaika kutafuta karatasi zenye maelezo
ya muungano huo, wanapoteza muda na kwamba mchakato wa katiba mpya usipewe
nafasi ya kuuangamiza taifa hili.
Kauli hiyo aliitoa leo mara baada ya kumalizika
kwa ibada ya kusimikwa kuwa Askofu mkuu wa jimbo hilo, ambalo lilikuwa wazi baada ya kujiuzulu
aliyekuwa Askofu wake Norbert Mtega mwaka mmoja uliopita.
Mhashamu Dallu alisema kila mtanzania anaowajibu mkubwa
wa kuhakikisha anatenga muda wa kuliombea taifa lake hasa
wakati huu ambao mchakato wa katiba mpya unaendelea, kwani bila kufanya hivyo
kutakuwa na uwezekano mkubwa wa kuwapa mwanya maadui ambao kimsingi hawaonyeshi
kulitakia mema taifa hili.
“Imepita miaka hamsini tukiwa pamoja hivyo tusikubali
kuvurugwa na watu wachache, anayetafuta katiba mpya kwa manufaa yake binafsi
hapaswi kuungwa mkono hata kidogo lazima katiba izingatie matakwa ya watanzania
wote na sio kikundi cha watu wachache wanaodhani kupatikana kwa aina fulani ya
katiba kutawanufaisha”, alisema Dallu.
Alieleza kuwa uwepo wa katiba mpya haimaanishi
matatizo ya watanzania yatakuwa yamemalizika, hivyo iwe katiba ya zamani au
inayoendelea kutafutwa kama wananchi hawatashirikiana na serikali yao kikamilifu katika
kujiletea maendeleo hali itabaki ileile.
Aidha alisisitiza kuwa kanisa katoliki litaendelea
kushirikiana na serikali katika kuendeleza shughuli za kijamii ambapo
itaendelea kujenga zahanati, vituo vya afya, hospitali na shule ili jamii iweze
kupata huduma hizo jirani kutokana na ukweli kwamba binadamu anamahitaji ya
kimwili na kiroho.
Awali Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Anne Makinda, aliwaasa watanzania juu ya umuhimu wa kufanya kazi ili
kuondokana na utegemezi ambao kimsingi umekuwa ni kikwazo katika kujiletea
maendeleo, iwe ya pamoja au ya mtu mmoja mmoja.
Makinda alisema serikali inathamini mchango mkubwa
unaotolewa na taasisi mbalimbali hapa nchini hususani za dini, hivyo itaendelea
kutoa ushirikiano wa dhati ikiwemo kuandaa mazingira mazuri ambayo hayatakuwa
kikwazo pale ambapo taasisi hizo zinataka kuwekeza kwa ajili ya kuwanufaisha
wananchi.
Aliwataka watanzania kuwa makini na watu wenye tabia
ya kuwashawishi wasijishughulishe kimaendeleo kwani kufanya hivyo itakuwa hawawatakii
mema, kutokana na kauli zao zisizo za msingi kuwa serikali ndiyo yenye jukumu
la kufanya kila kitu kwa ajili ya maendeleo ya wananchi wake.
No comments:
Post a Comment