Na Kassian
Nyandindi,
Songea.
CHAMA cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Songea mkoani Ruvuma,
kimewataka viongozi wake kuacha kufanya kampeni kabla ya wakati na
atakayebainika hatua kali za kisheria, zitachukuliwa ili iwe fundisho kwa
wengine wenye tabia kama hiyo.
Sambamba na hilo kimewataka kuepukana na makundi, na badala
yake kupitia mikutano ya wananchi waeleze utekelezaji wa ilani ya CCM ili
kuweza kujenga misingi ya kukiimarisha chama, na wananchi waweze kutambua nini
kimewafanyia.
Rai hiyo ilitolewa na Katibu wa Chama cha Mapinduzi wilaya ya
Songea, Josephat Ndulango alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini
kwake juu ya mikakati ya kukiimarisha chama hicho.
Ndulango alisema Watendaji katika maeneo mbalimbali wilayani
humo baadhi yao wamekuwa kikwazo katika kusukuma mbele maendeleo ya wananchi, hivyo
wamesisitizwa kuacha kujiingiza kwenye mambo ya kisiasa badala yake wazingatie
majukumu yao ya kazi.
“Malalamiko mengi tuliyoyapata watendaji wengi ni kuwa
wabadhirifu katika miradi ya wananchi, tumefuatilia na hatua zimeanza
kuchukuliwa ili kukomesha hali hii isiweze kuendelea na wananchi waweze
kunufaika na miradi yao”, alisema.
Pamoja na mambo mengine aliwaasa wananchi waache mambo ya
ushabiki wa kisiasa, wawe tayari kuchangia nguvu zao katika miradi ya maendeleo
kwa faida yao ya kizazi cha sasa na kijacho.
“Hatuko tayari kuona miradi ya maendeleo inashindwa kusonga
mbele kwa sababu ya mambo ya kisiasa, ni wakati sasa wa kujituma na sio kukaa
muda mwingi kulumbana pasipo faida yoyote”, alisema Ndulango.
Hata hivyo Katibu huyo alifafanua ni vyema katika uchaguzi
ujao wa serikali za mitaa, wananchi waanze kufikiria kuanzia sasa juu ya kupata
viongozi bora na waache tabia ya kuwaweka viongozi madarakani kwa majaribio.
No comments:
Post a Comment