Na Muhidin Amri,
Mbinga.
MKUU wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma,
Senyi Ngaga amegeuka mbogo na kuwaweka kiti moto baadhi ya vigogo wa wilaya
hiyo kufuatia kuwepo kwa matokeo mabaya, yaliyopatikana kwenye maeneo wanayo yaongoza
katika mtihani wa kumaliza elimu ya msingi mwaka jana.
Ngaga alisema hali hiyo imesababisha
wilaya hiyo kushika nafasi ya pili kimkoa kinyume na maadhimio waliyojiwekea
ya kushika nafasi ya kwanza katika mtihani huo.
Hali hiyo ilijitokeza wakati wa
kikao cha tathimini ya elimu ambapo Mkuu huyo wa wilaya hakuridhishwa na hali
ya ufaulu katika kata zinazoongozwa na vigogo hao ambao ni Mwenyekiti wa chama
cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Mbinga Christantus Mbunda, ambaye ni diwani
wa kata ya Mbangamao.
Vilevile Mwenyekiti wa Halmashauri ya
wilaya hiyo Allanus Ngahy diwani wa kata ya Kipapa na diwani wa kata ya Ngima Winfrid Kapinga ambaye
ni makamu Mwenyekiti wa halmashauri hiyo ambaye pia ni diwani wa kata ya Ngima wote
kupitia tiketi ya chama hicho.
Ngaga aliwataka viongozi hao watoke mbele wakiambatana na maafisa tarafa, walimu wa kuu wa shule zilizofanya vibaya pamoja na watendaji wa kata ambazo nazo zilichemsha katika matokeo hayo na kuwaita viongozi hao mbele ya wajumbe wengine wa kikao hicho ili waeleze sababu iliyofanya kata zao kupata matokeo mabaya huku wao wakiwa viongozi wa ngazi ya juu katika wilaya hiyo.
“Jamani nimewaita mbele siyo kwa
lengo la kuwahukumu au kuwafedhehesha hapana…….. bali ninachohitaji
kusikia kutoka kwenu nyinyi wenyewe sababu kubwa iliyowafanya mpate matokeo
mabaya katika kata zenu mkiwa viongozi tena wa ngazi
ya juu katika wilaya yetu, matokeo haya hayaridhishi hata kidogo hivyo
ni lazima wote kwa pamoja tutafute njia ya kumaliza tatizo hili kwani ni
kinyume na maadhimio yetu ya mwaka uliopita”, alisema Ngaga.
Katika matokeo hayo kata ya Mbangamao
ambayo diwani wake ni Mwenyekiti wa Chama cha mapinduzi ilishika
nafasi ya mwisho katika matokeo hayo kiwilaya kwa kupata alama 20
ambayo ni chini ya wastani unaotakiwa huku ikifuatiwa na kata ya Ngima
na Kipapa ambazo nazo zilipata alama chini ya 11 hivyo kuwa
miongoni mwa kata zilizofanya vibaya zaidi katika mtihani huo wa kumaliza elimu
ya msingi kitaifa.
Kata nyingine zilizofanya vibaya
zaidi ni Nanswea, Kipata, Kitanda, Kihangamahuka, Kihungu, Mpepai, Mbuji na
kata ya Kitumbalomo ambapo Mkuu huyo wa wilaya aliwataka viongozi wa kata
hizo kueleza sababu kubwa iliyopelekea kata zao kuvurunda ili kupata
majawabu ya kumaliza tatizo hilo la ufaulu kwa kuwa matokeo hayo yanaitia
aibu wilaya hiyo.
Aliwaagiza kuhakikisha wanamaliza
changamoto zilizosababisha kupata matokeo mabaya, ili mwakani ziweze kufanya vyema
na kuisogeza wilaya ya Mbinga hadi nafasi ya kwanza kimkoa jambo ambalo kwa
mujibu wa Mkuu huyo wa wilaya linawezekana kutokana na rasilimali
mbalimbali zilizopo.
Licha ya kuwataka watoe sababu
za kufanya vibaya lakini pia kueleza mikakati waliyonayo
kukabiliana na tatizo la utoro, ukosefu wa chakula cha mchana, nyumba za
walimu, madarasa na hata matundu ya vyoo ambazo zimeonekana kuwa ni moja
ya tatizo la kufanya vibaya katika mitihani iliyopita.
Aidha katika kikao hicho, ambacho
kilivutia wajumbe wengi kutokana na namna mkuu huyo wa wilaya
pamoja na wajumbe walivyokuwa wakichangia hoja zao, walishindwa kuficha
hisia zao kwa kumpongeza afisa elimu ya msingi Daud Mkali kutokana
ubunifu wake hasa katika kuanzisha makambi kwa watoto wa darasa la nne na
saba, pamoja na shule zilizofanya vizuri ambapo shule sita kati ya kumi bora kimkoa
zimetoka katika wilaya ya Mbinga.
No comments:
Post a Comment