Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
WANAFUNZI wa shule ya
sekondari Agustivo iliyopo katika wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma,
wametakiwa kuongeza juhudi katika masomo yao ili waweze kutimiza malengo waliyonayo
katika maisha na kuacha kujiingiza kwenye mambo yatakayowaharibia malengo yao.
Ushauri huo umetolewa na
mfanyabiashara maarufu mkoani Ruvuma Abbas Herman, alipokuwa
akizungumza na wazazi na wanafunzi kwenye mahafali ya kidato cha sita
shuleni hapo huku akisisitiza umuhimu wa elimu.
Katika sherehe hizo za kuwaaga
wahitimu wa kidato cha sita, mfanyabiashara huyo pia aliwazawadia wanafunzi 14
kiasi cha shilingi 25,000 kila mmoja waliokuwa wamefanya
vizuri katika masomo yao na kiasi cha shilingi 1,000,000 kwa ajili ya
shule hiyo ikiwa ni zawadi ya kufanya vizuri kitaaluma mkoani Ruvuma.
Alisema wilaya ya Mbinga ni kati ya
wilaya chache hapa nchini zenye fursa nyingi ambazo zinatoa nafasi kwa vijana
kujiendeleza zaidi kielimu, kwani hata historia inaonesha kuna idadi kubwa ya
viongozi waliosoma na kushika nafasi za juu hapa nchini lakini tatizo baadhi ya
vijana wenyewe hawataki kujituma na kuzingatia masomo yao.
“Nawasihi sana vijana ongezeni
juhudi katika masomo yenu, na nyinyi tunaowaaga leo hakikisheni mnatumia muda
huu kujiandaa na masomo ya juu zaidi badala ya kuridhika na hapa mlipofikia
kwani kumbukeni elimu haina mwisho”, alisema Abbas.
Aliongeza kuwa serikali kwa
kushirikiana na wadau wengine wa maendeleo imeanza kufungua milango ya
uwekezaji, hivyo inahitaji wasomi wengi watakaofanya kazi katika sekta
mbalimbali na ambao wanaelimu ya juu.
Hata hivyo aliwataka kujitambua na kuelewa kuwa vijana ndiyo
nguzo kuu ya uchumi katika nchi, kwa hiyo ni vyema wasome kwa bidii ili taifa
lipate wasomi wengi zaidi na wazalendo jambo ambalo litasaidia kuwa na
wataalamu wengi na kuokoa kiasi kikubwa cha fedha wanacholipwa wataalamu wa
fani mbalimbali wa nje.
No comments:
Post a Comment