Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu. |
Na Mwandishi wetu,
Mbinga.
BAADHI ya wakazi wa
wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma wameshauri na kulitaka Jeshi la polisi mkoani
humo, lijiepushe kufanya kazi zake kwa kusikiliza majungu na maneno ya
fitina katika utendaji wake wa kazi za kila siku na endapo wasipozingatia hilo,
mwisho wa siku huenda jeshi hilo linaweza kujikuta likabaki na askari wachache
wasiokuwa na sifa au weledi.
Ushauri huo
ulitolewa kwa nyakati tofauti walipokuwa wakizungumza na waandishi wa habari
mjini hapa, kufuatia kuwepo kwa malumbano yasiyokuwa na ulazima ambayo
yanaendelea kati ya baadhi ya vigogo ngazi ya wilaya na askari polisi.
Walieleza kuwa hali
hiyo imesababisha hata baadhi yao
kutoelewana ambapo kigogo mmoja ambaye ni Ofisa usalama wa taifa (jina tunalo)
na Mkuu wa polisi wa wilaya ya Mbinga (OCD) Justine Joseph wanadaiwa
kutoelewana na Mkuu wa kituo cha polisi wilayani humo Geofrey Ng’humbi.
Walisema malumbano
ya vigogo hao hayana faida katika jamii na yanatokana na Ng’humbi kufanya kazi zake kwa kuzingatia utawala
bora, hivyo kuonekana kuwa mwiba kwa wenzake.
Uchunguzi
uliofanywa na timu ya Waandishi wa habari umebaini kuwa viongozi hao wa ngazi
ya juu wilayani hapa ambao wanalalamikiwa ndio wanaodaiwa kujenga fitina,
majungu na njama za hapa na pale huku mambo ya chini kwa chini yakisukwa na
kusababisha Mkuu huyo wa kituo cha polisi Mbinga, aonekane kwamba ni tatizo hatimizi
majukumu yake ya kazi ipasavyo na kusababisha ahamishwe kwenda makao makuu ya
polisi mkoani Ruvuma yaliyopo Songea mjini.
Vilevile walieleza
kuwa ni vyema serikali ikachunguza jambo hili kwa makini, na ikiwezekana
uhamisho huo ufanywe kwa hata jeshi nzima la polisi wilayani Mbinga kwa ngazi
ya viongozi, kwa kile walichodai kuwa mkuu huyo wa polisi wa wilaya hiyo amekuwa
akishirikiana na ofisa huyo wa usalama kujenga uonevu kwa wananchi wa kawaida
ambao hawana tatizo lolote.
Kwa mujibu wa
malalamiko yaliyotolewa katika kikao kati ya Mkuu wa wilaya ya Mbinga Senyi
Ngaga na Madereva wa Pikipiki wilayani humo, ambacho kiliketi hivi karibuni
kwenye ukumbi wa Jumba la maendeleo mjini hapa walisema licha ya Ngaga
kufikishiwa ofisini kwake malalamiko yao
dhidi ya vigogo hao hawaoni utekelezaji uliozaa matunda.
Madereva hao
walieleza kuwa endapo hatua husika zisipochukuliwa wapo tayari kwenda ngazi ya
juu, ili waweze kupeleka malalamiko yao
na yaweze kufanyiwa kazi.
“Mheshimiwa mkuu wa
wilaya, sisi tupo tayari kwenda ngazi ya juu, maana inaonekana hapa hakuna
muafaka tuliofikia kwa sababu muda mwingi umekuwa ukiwatetea hawa watu wakati
sisi wanatunyanyasa”, alisema Bern Mangeni Katibu wa umoja wa waendesha
pikipiki wilayani Mbinga. (UWAMBI)
Waendesha pikipiki
hao ambao walionesha kukerwa na hali hiyo walizidi kumnyoshea kidole ofisa
usalama huyo wakidai kwamba hata uendeshaji wa gari lake la ofisi awapo
barabarani sio wakistaarabu, ambapo muda mwingi
amekuwa akiendesha kwa mwendo kasi hata akiwa hapa mjini na kunusurika kusababisha
ajali au kugonga watu.
Walisema kama ataendelea
kufanya hivyo itakuwa sio busara kwa kiongozi wa serikali kama
yeye ambaye amepewa dhamana kubwa ya kuhakikisha wananchi wa Mbinga wanakuwa
katika hali ya usalama, hivyo ni vyema arakebishe tabia hiyo na kuleta taswira
nzuri katika jamii.
Kwa upande wa OCD
Justine Joseph walifafanua kuwa aache kujenga makundi yasiyokuwa ya lazima kwa
jeshi la polisi wilayani humo, na endapo tatizo hilo litaendelea walitishia wakisema watadhamiria
kugomea shughuli mbalimbali za maendeleo ikiwemo suala la polisi jamii na
ulinzi shirikishi.
Walifafanua kuwa
wamepanga kwenda kumuona Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu na Kamanda wa
polisi wa mkoa huo, Kamishina msaidizi wa polisi Akili Mpwapwa ili kumueleza
masikitiko yao juu ya tabia na mienendo ambayo inaendelea kufanywa na viongozi
hao wilayani Mbinga.
“Tutaenda kumuona
mkuu wa mkoa tunajua ni kiongozi shupavu na mpenda haki licha ya kuelezwa
majungu mengi juu ya mgogoro huu unaoendelea hapa Mbinga, tunaamini
amedanganywa hakuna ukweli halisi aliopewa mezani kwake juu ya mahusiano mabaya
ya viongozi hawa wawili”, walisema.
Hata hivyo katika
kikao hicho hapakufikiwa muafaka wowote kutokana na waendesha pikipiki hao,
kuonekana kuja juu na kutoridhika na mwenendo mzima wa mambo wanayofanyiwa.
Nao baadhi ya
askari ambao pia hawakutaka kutaja majina yao wamesikitishwa na hatua ya jeshi
la polisi mkoani humo kumuhamisha Mkuu wa kituo cha polisi wilayani humo,
Geofrey Ng’humbi ambaye walisema alikuwa msaada mkubwa kwao kwa kila jambo, na sababu
za kumhamisha kwake walieleza kwamba ni kwa mtindo wa majungu na hawaoni sababu
ya msingi badala yake ni uonevu na mbinu ambazo zilipangwa na watu wachache.
Waliongeza kuwa
uongozi husika wa polisi ungefanya busara kama ni uhamisho
kuwaondoa wote hao lakini siyo ilivyofanya kumuhamisha mtu mmoja kwani
haukumtendei haki japo kuwa uhamisho ni sehemu ya mtumishi wa umma.
No comments:
Post a Comment