Na
Kassian Nyandindi,
Mbinga.
MWENYEKITI
wa Jumuiya ya Wazazi Taifa Alhaj Abdallah Bulembo, amemwagiza Mkuu wa wilaya ya
Mbinga mkoani Ruvuma, Senyi Ngaga kuhakikisha kwamba wilaya hiyo inaweka
mikakati madhubuti ya kuhamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi kupima afya
zao.
Agizo
hilo lilifuatia baada ya kusomewa taarifa ya maendeleo ya wilaya hiyo katika
ukumbi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilayani humo, ambayo ilionesha kwamba watu
300,000 tu ndio waliopima afya zao katika kipindi cha mwaka 2013 hadi mwaka
huu, ili waweze kujitambua kama wana maambukizi ya virusi vya ukimwi kiasi
ambacho ni kidogo kutokana na wilaya hiyo kuwa na watu wengi.
“Nimegundua
hapa hamasa ya upimaji VVU ni ndogo ukizingatia kwamba Mbinga kuna watu wengi
sana, kuanzia sasa tengenezeni hili liwe kama agenda katika vikao vyenu sio
tuna kaa kimya tuweke mazingira ambayo yenye programu ya muda mrefu na
endelevu”, alisema Bulembo.
Aidha
kwa wilaya hiyo kasi ya maambukizi ya ugonjwa huo imekuwa kubwa ambapo imefikia
asilimia 7 tofauti na takwimu za kitaifa asilimia 5, hivyo jitihada za makusudi
zinahitajika ili kuweza kupunguza kasi hiyo.
Pamoja
na mambo mengine Mwenyekiti huyo aliutaka uongozi wa wilaya ya Mbinga kupitia
idara yake ya afya, kuweka utaratibu wa kusambaza kondomu kwenye nyumba za
kulala wageni na suala hilo liwe la lazima na sio hiari.
“Hoja
ya kuwa na kondomu katika kila nyumba za kulala wageni halina mjadala hususan
kwa hapa mjini, ni jambo ambalo mnapaswa kuliweka katika mikakati yenu ya
wilaya kufanya hivi tunaweza kupunguza kasi hii ya maambukizi”, alisema.
Kwa
upande wake akijibu hoja za Mwenyekiti huyo wa Wazazi Taifa, Mkuu wa wilaya ya
Mbinga Ngaga alisema atatekeleza hilo haraka kwa kushirikiana na timu yake ya
wilaya, ikiwemo kuweka mikakati ya kuhamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi
kupima afya zao na kuwapa elimu juu ya maambukizi ya ugonjwa wa ukimwi.
No comments:
Post a Comment