Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete. |
Na Mwandishi wetu,
Mbinga.
IMEBAINIKA kwamba kumekuwa na mgogoro mzito unaoendelea kufukuta wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, kufuatia kuwepo kwa malumbano yasiyokuwa na ulazima, kati ya baadhi ya vigogo ngazi ya wilaya hiyo, askari polisi na madereva wa pikipiki.
Hali hiyo imefikia
hatua kwa baadhi yao kudaiwa kunyanyasa madereva wa pikipiki wa wilaya hiyo
huku uongozi wa umoja wa madereva hao (UWAMBI) uliopo wilayani hapa, ukijipanga
kwenda kwa mkuu wa mkoa huo Said Mwambungu ili waweze kufikisha kilio chao.
Ukweli juu ya mgogoro
huo ulijitokeza hivi karibuni katika kikao kilichoketi Mei 22 mwaka huu mjini
hapa, endelea kufuatilia mkasa huu kama
ifuatavyo;
UWAMBI wanena
kwenye kikao hicho:
Kwa mujibu wa
maelezo yaliyotolewa na Katibu wa umoja huo Bern Mangeni mbele ya mkuu wa
wilaya ya Mbinga Senyi Ngaga, kwa niaba ya wanachama wenzake alisema wamekuwa
wakinyanyaswa na Ofisa mmoja wa usalama wa taifa wilayani hapa (jina tunalo) na
Mkuu wa polisi wa wilaya hiyo Justine Joseph.
“Mheshimiwa mkuu wa
wilaya sisi tutaendelea kusonga mbele ngazi ya juu kwa sababu inaonesha
umeshindwa kutusaidia, tumebaki kwenye hali ya sintofahamu juu ya tatizo hili”,
alisema Bern Mangeni.
Walalamikia juu ya Manyanyaso:
Mangeni katika
kikao hicho anasema Ofisa huyo wa usalama anadaiwa kumgonga mjini hapa dereva wa pikipiki Hassan Said,
kutokana na uendeshaji wa gari lake la ofisi awapo barabarani sio wakistaarabu,
huku muda mwingi amekuwa akiendesha kwa
mwendo kasi hata akiwa katika maeneo ya hapa mjini.
Alieleza kuwa baada
ya kumgonga alipiga simu polisi kwa lengo la kuita askari waje wamkamate
dereva huyo wa pikipiki, huku akiwa amemkamata na kumtolea vitisho vya hapa na
pale kwamba dereva huyo wa pikipiki alikuwa na makosa barabarani wakati sio
kweli, ambapo askari hao walipowasili eneo la tukio walimchukua Hassan Said na
kwenda kumweka mahabusu.
Ushuhuda watolewa:
Katika kikao hicho
Hassan Said alitoa ushuhuda mbele ya mkuu wa wilaya hiyo Senyi Ngaga ambapo
alisema wakati anagongwa na gari na Ofisa usalama huyo, alishuka katika gari lake na
kumkamata kisha kumtandika makofi, huku akimtishia na silaha aliyoitaja mbele
ya kikao hicho kuwa ni bastola.
Wakati tukio hilo
likiendelea alisema alikuwa akipiga simu akiita askari polisi waje eneo la
tukio ambao baada ya kuwasili walimkamata dereva huyo wa pikipiki na kumweka
mahabusu kwa siku mbili, huku dhamana ikizuiliwa hadi alipopelekwa Mahakamani
ambako nako ilikuwa ni tatizo kupewa dhamana na akaishia kusota mahabusu kwa
muda wa miezi miwili huku kesi yake akihudhuria mahakamani kwa kadiri ya siku
ilivyokuwa ikitajwa hadi alipohukumiwa.
Hassan Said alisema
wakati kesi inaendelea katika mahakama ya wilaya ya Mbinga licha ya kueleza
ukweli juu ya tukio lenyewe, ilishindikana kuweza kujinasua kutokana na mpango
mchafu uliopangwa wa kuendelea kumkandamiza aishie jela.
“Mheshimiwa Mkuu wa
wilaya askari mmoja ambaye namtambua kwa jina moja la Seif, alikuja kwangu na
kuniambia kwamba afisa usalama alikuwa anataka hela ili aweze kufuta kesi
ambayo ilifunguliwa kule mahakamani,
“Mimi mwenyewe
niliwasiliana na ndugu zangu wakati nikiwa bado mahabusu niliwaagiza wauze
baadhi ya vitu vyangu; kitanda changu cha kulalia, godoro, redio, Tv, ili niweze
kupata fedha nijinasue na mkasa huu”, alisema Hassan Said.
Alifafanua kuwa
baada ya ndugu zake kuuza vitu hivyo wakati yeye akiwa bado mahabusu, waliweza
kufanikiwa kupata fedha tasilimu shilingi 500,000 ambazo baadae alikabidhiwa
askari huyo aliyemtaja kwa jina la Seif, ili akazipeleke kwa Ofisa usalama huyo
na yeye aweze kujinasua katika kesi hiyo.
Lakini cha
kushangaza licha ya kutoa fedha hizo hakuna kitu kilichoendelea, zaidi ya yeye
kuendelea kusumbuka na kesi ambayo ilikuwa ikimkabili na hatimaye aliishia kwenda
kutumikia kifungo jela miezi sita.
Vilevile alisema mkasa
huo alikumbana nao mwaka 2012 ambapo alisota mahabusu kwa miezi miwili hadi kesi
yake ilipohukumiwa na kufungwa tena jela miezi sita, na baadaye alipomaliza kifungo
chake alirudi nyumbani kuendelea na majukumu yake ya kazi za kila siku.
Mlalamikaji:
Wakati Hassan Said
anatoa malalamiko hayo mbele ya Mkuu wa wilaya ya Mbinga, bado alionekana
kutoeleweka ambapo Ngaga alikuwa akionesha kuendelea kumtetea kiongozi huyo
wa usalama ambaye amepewa dhamana ya kushikilia mhimili wa dola wilayani humo, kuhakikisha
kwamba wananchi wake wanakuwa salama wakati wote.
Mkuu wa polisi
wilaya ya Mbinga:
Madereva hao wa
pikipiki walizidi kutoa malalamiko yao
dhidi ya askari wa barabarani, ambapo walisema wamekuwa wakitozwa faini za
makosa ya barabarani bila kukatiwa stakabadhi (risiti).
Walisema pamoja na
kufikisha kilio chao kwa mkuu wa polisi wa wilaya hiyo Justine Joseph hakuna
utekelezaji unaonesha kuzaa matunda, badala yake muda mwingi anaonekana
kuwatetea askari wake pale anapofikishiwa malalamiko.
Diwani kata ya
Mbinga mjini athibitisha:
Aidha pamoja na
Diwani wa kata ya Mbinga mjini Kelvin Mapunda kuthibitisha juu ya matukio
wanayotendewa madereva hao wa pikipiki wilayani humo, bado alionekana
kutoeleweka na Mkuu wa wilaya hiyo Senyi Ngaga na kufikia hatua kikao hicho kuvurugika
na kutofikia muafaka.
Mkuu wa wilaya ya
Mbinga:
Baada ya Diwani
huyo kuonesha kwamba anaeleza ukweli juu ya tukio hilo, Senyi Ngaga alikuwa na jazba huku
akisema “diwani leo unanisaliti...............” na kwamba kufuatia hali hiyo kikao hicho
ambacho kilidumu kwa muda wa masaa manne kilivunjika bila kupatiwa ufumbuzi.
No comments:
Post a Comment