Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
IDARA ya Maendeleo ya Jamii katika Halmashauri ya wilaya ya
Mbinga mkoani Ruvuma, imezinyoshea kidole baadhi ya asasi zisizo za kiserikali
wilayani humo kwamba, hazitekelezi majukumu yake ya kazi ipasavyo.
Sambamba na hilo imeelezwa kuwa taarifa za kazi inazofanya
hazitolewi kabisa juu ya nini asasi husika inafanya, jambo ambalo ni kinyume na
taratibu zilizowekwa wakati zinasajiliwa na kupewa majukumu ya kwenda
kuyafanya.
Kauli hiyo ilitolewa na Ofisa maendeleo ya jamii Henry
Digongwa anayeshughulikia kitengo cha UKIMWI na tiba, katika halmashauri hiyo alipokuwa
kwenye mkutano wa siku mbili na Wadau wa mapambano dhidi ya ugonjwa huo, uliofanyika
ukumbi wa shule ya sekondari Kigonsera iliyopo wilayani humo.
“Ndugu zangu kazi ya asasi ni kuisaidia serikali katika
kutekeleza majukumu yake, taarifa hazitolewi kabisa juu ya nini mnakifanya
nahitaji mbadilike”, alisema Digongwa.
Digongwa alisisitiza kuwa hivi sasa umewekwa utaratibu
kwamba, asasi ambayo itakuwa haiwajibiki ipasavyo katika maeneo yake ya kazi na
kutoa taarifa zake kwa wakati, zitafutiwa usajili wake.
Awali akifungua mkutano huo, Ofisa maendeleo ya jamii wa
wilaya ya Mbinga, Paschal Ndunguru naye alizitaka asasi zisizo za kiserikali
wilayani humo kujenga ushirikiano wa kazi zao na serikali, na sio kusubiri
mpaka wasukumwe.
“Tuwajibike kwa yale ambayo tumejiwekea sisi wenyewe, kazi yenu
ndugu zangu mnatakiwa kupembua matatizo ambayo jamii inayowazunguka
inakabiliana nayo”, alisema.
Hata hivyo aliongeza kuwa kazi ya serikali ni kuona asasi
hizo, zinaendelea kuelimisha jamii katika kupambana na ugonjwa wa UKIMWI ili
kuweza kupunguza kasi ya maambukizi ya ugonjwa huo.
No comments:
Post a Comment