Na Kassian Nyandindi,
Nyasa.
SIMANZI
na majonzi vilitawala katika mji mdogo wa Mbamba bay wilayani Nyasa mkoa wa
Ruvuma, kufuatia wanafunzi wawili wakazi wa mji huo wanaosoma shule ya msingi
Mbamba bay wilayani humo kufariki dunia, baada ya kuteketea kwa moto katika
chumba walichokuwa wamelala ambacho inadaiwa kuwa walifungiwa nje kwa kufuli na
kuwafanya washindwe kujiokoa.
Kwa
mujibu wa vyanzo vya uhakika vya habari vimeeleza kuwa tukio hilo lilitokea Mei
23 mwaka huu majira ya usiku, ambapo chanzo cha moto huo hadi sasa hakijulikana
na kwamba watoto hao walifungiwa kwenye chumba ambacho ni duka la bidhaa
mbalimbali ambalo vitu vilivyokuwa ndani yake navyo viliteketea kabisa.
Watoto
waliokumbwa na mkasa huo ni Sharifa Nurudin (13) ambaye anasoma darasa la saba
na Ismail Nurudin (11) wa darasa la tano katika shule hiyo, imedaiwa kuwa
walikuwa wakifungiwa mara kwa mara kwenye duka hilo lenye jina maarufu ‘Kwa
mjomba Nuru’ nyakati za usiku, kwa lengo la kulinda mali zilizomo ndani
yake.
“Watoto
hawa walikuwa siku zote wanafungiwa nje na kufuli na baba yao mzazi Nurudin
Mohamed, licha ya watu kumweleza acha kuwatumikisha watoto hawa kwa mtindo huu
alikuwa hataki kusikia na leo watoto wamepoteza maisha kwa sababu ya ujinga wa
huyu baba”, alisema mama mmoja mkazi wa mji mdogo wa Mbamba bay ambaye hakutaka
jina lake litajwe gazetini.
Wakizungumza
kwa nyakati tofauti na mwandishi wa habari hizi wakazi wa mji huo walifafanua
kuwa watoto hao walikuwa wanaishi na mama yao wa kambo, waliyemtaja kwa jina la
Anna Pilly ambapo muda mwingi walikuwa wakitumikishwa kufanya kazi ngumu na
kukosa malezi bora.
Walibainisha
kuwa walikuwa wakiishi na mama huyo katika mazingira magumu, baada ya mama yao
mzazi Fulale Msumba ambaye hivi sasa anaishi Songea mjini, kuachana na huyo
baba yao miaka kadhaa iliyopita.
Mazishi
ya miili ya watoto hao imefanyika katika makaburi yaliyopo hapo Mbamba bay Mei
24 mwaka huu, majira ya mchana.
Aidha
Kamanda wa polisi wilayani Nyasa Amiri Mganga hakuweza kupatikana ofini kwake,
lakini alipoulizwa kwa njia ya simu alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na
kusema kuwa hawezi kutolea maelezo ya kina kwa sababu yupo katika ziara ya
kikazi.
“Unajua
hivi sasa unavyonipigia nipo kati kati ya ziara ya katibu wa wazazi taifa,
nitashindwa kukupatia maelezo juu ya jambo hili tupo na mgeni huyu wa chama cha
mapinduzi (CCM) hapa wilayani kwetu, naomba nitafute muda mwingine”, alisema
Mganga.
Hata
hivyo gazeti hili lilipozungumza na Kamanda wa polisi wa mkoa wa Ruvuma,
kamishina msaidizi wa polisi Akili Mpwapwa alisema kuwa yeye hana taarifa juu
ya tukio hilo, mpaka atakapowasiliana na mkuu huyo wa kituo cha polisi wilaya
ya Nyasa.
No comments:
Post a Comment