Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Taifa, Alhaj Abdallah Bullembo akihutubia leo mamia ya wakazi wa Mbinga mjini katika uwanja wa soko kuu mjini hapa. |
Aliyekuwa Mwenyekiti wa CHADEMA Desderius Haulle akiwa amebebwa na Wafuasi wa CCM baada ya kurejesha kadi ya chama hicho pinzani na kuhamia chama tawala. (Picha zote na Kassian Nyandindi) |
Mbinga.
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimepata pigo
wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, kufuatia aliyekuwa Mwenyekiti wake wa chama
hicho wilayani humo Desderius Haulle kujitoa uanachama na kuhamia Chama Cha Mapinduzi
(CCM).
Tukio hilo limejitokeza leo katika mkutano wa hadhara
uliofanyika kwenye uwanja wa soko kuu uliopo mjini hapa, ambao ulikuwa
ukihutubiwa na Mwenyekiti wa taifa wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi
Alhaj Abdallah Bulembo.
Sambamba na hilo katika mkutano huo pia alijitokeza mwanachama
mmoja wa Chama Cha wananchi CUF, Maria Ndimbo naye alirejesha kadi yake ya
chama hicho na kuhamia CCM.
Haulle alirudisha kadi ya CHADEMA na kukabidhiwa ya CCM,
ambapo alipopewa nafasi ya kuzungumza alisema amechoshwa na sera za chama hicho
pinzani ambazo hazina utekelezaji.
“Leo nimeamua kurejesha kadi hii na kuhamia katika chama hiki
tawala kwa sababu nafahamu mambo mengi yanayofanywa na CHADEMA, hivyo
nilivumilia kwa muda mrefu lakini leo imefikia mwisho wake naomba tuungane
pamoja tujenge taifa letu”, alisema Haulle.
Alisema chama hicho pamoja na kuitwa ni cha kidemokrasia,
hakuna ukweli wowote juu ya hilo na badala yake kimekuwa kikiendeshwa kiukabila
ambapo mtu au kiongozi yeyote anayetoka nje ya mikoa ya Kaskazini hathaminiwi
ndani ya chama hicho.
Pamoja na mambo mengine akihutubia mamia ya wananchi
waliokusanyika katika eneo la uwanja wa soko hilo mjini hapa, Bulembo
alimpongeza Haulle kufuatia uamuzi wake wa kurudi CCM chama ambacho kinafuata
misingi bora ya kidemokrasia bila ubaguzi.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti huyo wa Jumuiya ya Wazazi Taifa,
alisema ubinafsi na ukabila ndani ya CHADEMA umejionyesha wazi Bungeni ambapo
kila kiongozi aliye juu anaye ndugu yake ambaye ni Mbunge ndani ya bunge.
Bulembo aliwataka wananchi ambao wamepotea njia na kwenda
upinzani, warudi CCM kwani ndicho chama chenye sera zinazolenga kuwaletea
maendeleo ya kweli Watanzania na kudumisha amani na utulivu uliodumu tangu nchi
ilipopata uhuru.
No comments:
Post a Comment