Na Kassian
Nyandindi,
Mbinga.
TATIZO la mimba mashuleni kwa shule za msingi na sekondari
wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, lisipotafutiwa mbinu ya kudhibitiwa mapema,
hakika maendeleo katika sekta ya elimu wilayani humo huenda yakadorola.
Imefafanuliwa kuwa wazazi na walimu katika shule husika ndio
chanzo kikuu cha tatizo hilo ambapo kwa kiasi kikubwa, wamekuwa wakifumbia
macho kwa kutowachukulia hatua za kisheria watu wanaohusika kuwapatia wanafunzi
wa kike ujauzito.
Wadau wa elimu wilayani Mbinga mkoani humo, walisema hayo
mbele ya Mkuu wa wilaya hiyo Senyi Ngaga ambaye alikuwa Mwenyekiti katika kikao
cha tathimini ya elimu, kilichoketi katika ukumbi wa Jimboni uliopo mjini hapa.
Akizungumza katika kikao hicho Ngaga alionesha kusikitishwa
na tatizo hilo, ambapo alisema kwa mwaka wamekuwa wakipata kesi za mimba zaidi
ya 160 na hakuna mtuhumiwa hata mmoja anayekamatwa kutokana na wazazi kutotoa
ushirikiano wa kutosha katika vyombo vya sheria ambavyo vinashughulikia tatizo
hilo.
“Tatizo la mimba katika wilaya yetu ni kubwa mno ukijumlisha
kwa shule za msingi na sekondari, kwa mwaka tumekuwa tukizalisha mimba nyingi
haiwezekani watoto wetu wa kike wanaendelea kupewa mimba halafu tunakaa kimya”,
alisema Ngaga.
Mkuu huyo wa wilaya ya Mbinga, pia aliwanyoshea kidole
Watendaji wa vijiji na kata kwa kile alichoeleza kuwa, tatizo hilo la mimba
wamegeuza kama ni mtaji wao wa kujipatia fedha na kumaliza mambo kienyeji, huku
wakiacha kuwachukulia hatua wahusika.
“Wazazi tusikubali kurubuniwa kwa vijipesa vidogo vidogo
halafu watoto wetu wa kike wanaharibika kwa kukatisha masomo yao kutokana na
tatizo hili”, alisema.
Naye Mganga Mkuu wa wilaya ya Mbinga Damas Kayera alieleza
kuwa , watoto wengi wanaokwenda kujifungua katika hospitali ya wilaya hiyo ni
mabinti wadogo wadogo, ambao wamekatisha masomo yao shuleni kutokana na kupewa
ujauzito.
“Mheshimiwa mwenyekiti wa kikao hiki, kesi nyingi za mimba ninazozipokea
pale hospitali ni za watoto hasa wa kidato cha pili”, alisema Kayera.
Wadau hao wa elimu walijiwekea mkakati wa
kuhakikisha kwamba hatua madhubuti sasa zichukuliwe dhidi ya wahusika wenye
kusababisha tatizo hilo, ikiwemo kufikishwa Mahakamani ili iwe fundisho kwa
wengine wenye tabia kama hiyo.
No comments:
Post a Comment