Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Kassim Majaliwa. |
Na Kassian Nyandindi,
Ruvuma.
HATIMAYE Baraza la Madiwani katika
Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, limemaliza mzizi wa fitina kwa kumkataa aliyekuwa Ofisa elimu
wa wilaya hiyo Hanji Yusuph Godigodi na kusema kuwa hawataki kumuona ndani ya
wilaya hiyo, akiendelea kufanya kazi za utumishi wa umma.
Kukataliwa kwa Ofisa huyo kumefuatia
baraza hilo kuketi kama kamati kwa muda wa nusu saa kujadili suala hilo, likizingatia tamko
lililotolewa na Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Ofisi ya Waziri Mkuu
Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Kassim Majaliwa, Februari 7
mwaka huu wakati alipokuwa katika ziara yake ya kikazi wilayani humo.
Jukumu la kuketi kama kamati lilifuatia
kuwepo kwa mchezo mchafu ambao ulikuwa ukisukwa chini kwa chini na baadhi ya
vigogo wa ngazi ya mkoa huo na wilaya, kwa lengo la kutaka kumrejesha
madarakani Ofisa huyo ili aendelee na kazi yake kama kawaida.
Majaliwa alitoa tamko la kumvua
madaraka kwa kumshusha cheo Ofisa huyo
wa elimu sekondari wilayani humo, na wenzake sita ambao ni walimu wakuu wa
shule za sekondari, kufuatia kushindwa kutekeleza majukumu yao ya kazi na
kufanya ubadhirifu wa zaidi ya shilingi milioni 268 za maendeleo ya elimu ya
sekondari.
Sambamba na hilo aidha mtumishi mmoja
wa Mamlaka ya mji mdogo wa Mbinga ambaye ni Prosper Luambano naye amekataliwa
na baraza hilo kutokana na kutotekeleza majukumu yake ya kazi ipasavyo, na
kumtaka Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga kuchukua hatua
mara moja, ya kumhamisha kumpeleka kituo kingine cha kazi nje ya wilaya hiyo.
Maamuzi hayo ya kuwakataa Watumishi
hao yametolewa leo na Mwenyekiti wa Baraza la madiwani wa Halmashauri ya wilaya
ya Mbinga Allanus Ngahy, katika kikao cha baraza hilo kilichoketi kwenye ukumbi
wa Jumba la maendeleo mjini hapa.
Wakuu wa shule za sekondari wilayani
Mbinga ambao nao walivuliwa madaraka na Waziri Majaliwa na kushushwa vyeo vyao
ni William Hyera ambaye ni wa shule ya sekondari Maguu, Clemence Sangana
anatoka shule ya sekondari Mkuwani, Method Komba Langilo sekondari, John Tillia
Ukilo sekondari, Leonard Juma Luli Sekondari huku akimtaja kwa jina moja
mwalimu Konga ambaye yupo sekondari ya Kihangimahuka.
Kwa mujibu wa tamko hilo ambalo
lilitolewa na Waziri huyo aliagiza kuwa Ofisa elimu wa sekondari wa wilaya hiyo
Hanji Yusuph Godigodi na Wakuu wa shule hizo, anawavua madaraka waliyonayo kwa
kuwashusha cheo na kwenda kuwa walimu wa kawaida wakafundishe (Wakashike chaki)
darasani ili iwe fundisho kwa watumishi wengine ambao wenye utovu wa nidhamu,
na ambao hawataki kuzingatia maadili ya utumishi umma.
Kufuatia rungu hilo ambalo
limewaangukia watumishi hao, katika nafasi ya Ofisa elimu sekondari wilaya ya
Mbinga hivi sasa inashikiliwa na Lucy Mwalukyosa ambaye atakuwa kaimu Ofisa
elimu sekondari wa wilaya hiyo, na kwa upande wa shule za sekondari walimu ambao
walikuwa wasaidizi ndio watakao kuwa Wakuu wa shule hizo kama ilivyoagizwa na
Naibu Waziri wa TAMISEMI alipokuwa ziarani hivi karibuni wilayani Mbinga.
No comments:
Post a Comment