Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
UMOJA wa Wazazi wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, umewataka
wananchi wa wilaya hiyo kutunza na kuendeleza mazingira kwa maendeleo ya jamii
na taifa kwa ujumla.
Aidha imesisitizwa kuwa katika kufanikisha hilo, viongozi wa
serikali waliopo katika maeneo mbalimbali katika vijiji na kata wahakikishe
kwamba wanahamasisha watu kupanda miti iliyo rafiki ya maji, katika vyanzo vya
maji na vilele vya milima.
Rai hiyo ilitolewa na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)
wa wilaya ya Mbinga, Christantus Mbunda alipokuwa mgeni rasmi akihutubia katika
maadhimisho ya sherehe za umoja huo yaliyofanyika katika kijiji cha Mundeki
kata ya Myangayanga wilayani humo.
Mbunda alisisitiza pia watu waache tabia ya kukata miti ovyo
na kuagiza Watendaji wa vijiji na kata kusimamia sheria za utunzaji mazingira, kwa
kuwaelimisha wananchi na kuchukua hatua pale wanapoona uharibifu unafanyika.
Awali Mwenyekiti wa umoja wa Wazazi wilayani hapa, Imelda
Mapunda naye alisema kuna umuhimu kwa wazazi wa wilaya hiyo kuendelea kuweka
mkazo katika suala zima la elimu ikiwemo kupeleka watoto wa shule, na kutoa
michango kwa wakati.
Mapunda alisema usimamiaji kikamilifu katika utekelezaji wa
sera ya malezi mema kwa watoto na vijana ni jambo ambalo halipaswi kufanyiwa mzaha,
hivyo jamii iungane kwa pamoja katika kulitekeleza hilo.
Pamoja na mambo mengine alieleza kuwa msimamo wa chama na
jumuiya za CCM kwa pamoja kuhusu rasimu ya pili ya katiba, wao wanahitaji uwepo
wa serikali mbili za Jamhuri ya muungano nasio vinginevyo.
No comments:
Post a Comment