Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
MKUU wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Senyi Ngaga amewataka
Madiwani wa Halmashauri ya wilaya hiyo wasiwe watu wa kugeuka geuka, pale
wanapoweka misimamo au misingi muhimu ya maendeleo ya wananchi wa wilaya hiyo.
Ngaga alisema kuwa kumekuwa na baadhi ya Madiwani wamekuwa
wakishindwa kusimamia makubaliano halali ya vikao husika, badala yake muda
mwingi huishia kulumbana na kuzungumzia mambo ambayo hayana tija kwa wananchi.
Kauli hiyo ya Mkuu wa wilaya Mbinga, ilitolewa leo alipokuwa
akizungumza na Madiwani wa Halmashauri ya wilaya hiyo katika kikao cha baraza
la madiwani hao kilichoketi leo, kwenye ukumbi wa Jumba la maendeleo uliopo
mjini hapa.
“Hii tabia sipendi, tujenge misimamo yetu katika vikao tusiende
na manufaa ya mtu mmoja mmoja, tushirikiane katika hili ili mambo yetu yaende
vizuri”, alisisitiza.
Aidha Ngaga alilieleza baraza hilo kuwa kuanzia mwaka huu, baadhi
ya vijiji 34 vilivyopo wilayani humo serikali itajenga miundombinu ya umeme na
kwamba ifikapo mwezi Julai mwakani, kazi hiyo itakuwa imekamilika.
Katika vijiji hivyo 11 vitaunganishwa kwenye mtandao wa gridi
ya taifa na 23 vitaingia kwenye mradi wa umeme vijijini, ambapo taratibu husika
zimekwisha kamilika na kazi ya ujenzi wa miundombinu ya umeme wakati wowote kuanzia sasa itaanza
kujengwa.
“Ndugu zangu Madiwani hamasisheni wananchi wajenge
ushirikiano katika kuona umuhimu wa mradi huu wa umeme, na tutambue kwamba
hakuna atakayelipwa fidia yoyote kwenye maeneo ambayo mradi huu unapita,
tunachotakiwa tuelimishe wananchi wetu waweze kulielewa hili”, alisema Ngaga.
Pamoja na mambo mengine alikemea kitendo cha Watendaji wa
vijiji na kata kutosimamia ipasavyo ujenzi wa miradi ya wananchi, ambapo baadhi
yake kama vile majengo ya shule za msingi na sekondari yamejengwa kwa kiwango
cha chini jambo ambalo alisema ni ubadhirifu wa fedha za wananchi.
No comments:
Post a Comment