Monday, April 7, 2014

NMB YATOA MSAADA HOSPITALI NA SHULE YA MSINGI YA WATAKA WAZAZI KUWAFUNGULIA AKAUNTI WATOTO WAO

Meneja wa NMB Kanda ya kusini, Lillian Mwinula akisisitiza jambo wakati wa kukabidhi msaada wa madawati, shuka na vyandarua alipokuwa katika ziara yake ya kikazi wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma. Upande wa kushoto ni Meneja wa benki hiyo tawi la Mbinga Lugano Mwampeta na kulia ni Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri  ya wilaya ya Mbinga Oscar Yapesa.

Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma Oscar Yapesa upande wa kulia, akipokea msaada wa vyandarua kutoka kwa Meneja wa NMB Kanda ya kusini Lillian Mwinula.

Baadhi ya akina mama Wajawazito nao wakishuhudia makabidhiano ya vyandarua na mashuka katika hospitali ya wilaya ya Mbinga.

Upande wa kulia Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga Oscar Yapesa akipokea msaada wa madawati 50 kutoka kwa Meneja wa Kanda ya kusini wa NMB, Lillian Mwinula kwa ajili ya matumizi kwa wanafunzi wa shule ya msingi Komboa iliyopo kata ya Ruanda wilayani humo.

Wanafunzi wa shule ya Msingi Komboa wakiimba wimbo wa kushukuru mara baada ya kukabidhiwa madawati hayo.


Lillian Mwinula ambaye ni Meneja wa NMB Kanda ya kusini, akiwa pamoja na wanafunzi wa shule ya msingi Komboa mara baada ya kuwakabidhi madawati.

Wanafunzi wa shule ya msingi Komboa iliyopo kata ya Ruanda wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, wakiwa wameketi katika madawati hayo, mara baada ya kukabidhiwa na benki ya NMB. (Picha zote na Kassian Nyandindi)

Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.


BENKI ya NMB tawi la Mbinga mkoa wa Ruvuma, imetoa msaada wa Madawati 50 yenye thamani ya shilingi milioni tano kwa shule ya msingi Komboa iliyopo kata ya Ruanda wilayani humo, ikiwa ni lengo la kuboresha mazingira ya kusomea wanafunzi katika shule hiyo.

Sambamba na hilo pia imetoa msaada wa mashuka 30 na vyandarua 10 katika hospitali ya wilaya hiyo, kwa ajili ya akina mama wajawazito ambao husubiri siku ya kujifungua na kupata matibabu katika hospitali hiyo.

Akizungumza mara baada ya kukabidhi vitu hivyo Meneja wa benki hiyo Kanda ya kusini, Lillian Mwinula alisema NMB kila mwaka imejiwekea utaratibu wa kurudi kwa wananchi pale inapopata faida yake, kwa njia ya kutoa misaada ya aina mbalimbali.


Aidha alisema kuwa utaratibu huo unalenga kuisaidia jamii yenye hali ya chini kimaisha, ili iweze kuondokana na adha inayopata na hatimaye kusonga mbele kimaendeleo.

Mwinula aliwataka Wazazi wilayani Mbinga kuweka akiba katika benki hiyo, kwa kuwafungulia akaunti watoto wao ili waweze kujiendeleza kielimu.

“Ndungu zangu wazazi kuweni na mazoea ya kuweka akiba kidogo kidogo katika benki yenu ya NMB wafungulieni akaunti watoto wenu ili wajiendeleze kielimu zaidi”, alisema Mwinula.

Hata hivyo kwa upande wake kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga, Oscar Yapesa aliishukuru benki hiyo kwa msaada huo uliotolewa huku akitoa rai kwa taasisi na mashirika mbalimbali nchini kuwa na moyo wa kusaidia wananchi wenye kipato cha chini, ili waweze kuondokana na umasikini.




No comments: