Thursday, April 17, 2014

JELA MIAKA 30 KWA KOSA LA UBAKAJI



Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

MAHAKAMA ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, imemhukumu kwenda jela kutumikia kifungo cha miaka 30 mkazi mmoja wa kijiji cha Mhekela wilayani humo, baada ya kupatikana na kosa la kubaka msichana mwenye umri wa miaka 14.

Hukumu hiyo ilitolewa na Hakimu Joackimu Mwakyolo mbele ya mwendesha mashtaka msaidizi wa Polisi Inspekta Nassib Kassim ambapo ilielezwa Mahakamani hapo kuwa, ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka umeona kwamba mshtakiwa anastahili kupewa adhabu ya kwenda jela kutumikia kifungo hicho. 

Mwakyolo alisema Wilson Ndunguru (32) ambaye ni mshtakiwa wa kosa hilo, alimbaka msichana mwenye umri wa miaka 14 mkazi wa mtaa wa Jimboni Mbinga mjini.


Alisema binti huyo alimkamata kwa nguvu na kumvutia kichakani kisha kumuingia kimwili bila ridhaa yake na kwamba kabla ya kutolewa hukumu hiyo, Mahakama ilimpatia mshtakiwa nafasi ya kujitetea ambapo aliiomba isimhukumu adhabu kali kutokana na yeye ni mara yake ya kwanza kufanya kosa hilo lakini utetezi wake ulitupiliwa mbali. 

Awali mwendesha mashtaka msaidizi wa Polisi Inspekta Kassim, alisema tukio hilo lilitokea Septemba 22 mwaka jana majira ya saa tano asubuhi katika mtaa huo.

Kassim alifafanua kuwa mshtakiwa huyo wakati anafanya tendo hilo, pia alitumia nguvu kubwa kwa kumziba mdomo binti huyo ili asipige kelele kitendo ambacho kilimsababishia maumivu makali.

Hata hivyo mwendesha mashtaka huyo aliiomba Mahakama itoe adhabu kali kwa mshtakiwa ili iwe fundisho kwa wengine wenye kufanya vitendo kama hivyo, ambavyo wakati mwingine husababisha watu kuambukizwa magonjwa ya zinaa na hata Ukimwi.



No comments: