Na Kassian
Nyandindi,
Mbinga.
HALMASHAURI za wilaya mkoani Ruvuma zimeagizwa kuongeza
vyanzo vipya vya mapato, ambavyo vitaweza kusaidia kuendesha halmashauri hizo
na kuhudumia wananchi badala ya kutegemea ruzuku kutoka kwa wafadhili au
serikali kuu.
Agizo hilo lilitolewa na Mkuu wa wilaya ya Mbinga Senyi Ngaga
alipokuwa akifungua mkutano wa Jumuiya ya Serikali za Mitaa (ALAT) ambao ulifanyika juzi katika ukumbi wa
Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani humo.
Ngaga alisema viongozi wa Halmashauri wasipokuwa wabunifu katika
kuongeza mapato, hawataweza kwenda mbele na kutimiza malengo ya kuhudumia jamii
ikiwemo ujenzi wa miundombinu kama vile barabara na miradi ya kilimo.
“Tukijiongezea wigo wa mapato katika maeneo tunayowaongoza
wananchi wetu tutaweza kusonga mbele, ni vyema tuzingatie hilo”, alisema Ngaga.
Alisema Halmashauri ikitegemea chanzo kimoja cha mapato kufikia
malengo iliyojiwekea itakuwa ni vigumu, na kusababisha kushindwa kutoa huduma
husika kwa wananchi.
Pamoja na mambo mengine, Mkuu huyo wa wilaya ya Mbinga mkoani
Ruvuma alisisitiza pia uboreshaji wa kiwango cha elimu katika shule za msingi
na sekondari mkoani humo, ili kuufanya mkoa huo uweze kufikia malengo mazuri ya
ufaulu ambayo imejiwekea katika sekta hiyo.
“Natoa wito kwa viongozi wote na wananchi ndani ya mkoa wetu,
tushirikiane kuinua taaluma katika shule zetu, tuna kila sababu kuhakikisha
tunabadilisha taswira hii ya elimu tuliyonayo sasa na kufikia hali nzuri ya
ufaulu”, alisema.
Hata hivyo alieleza kuwa hali ya kiwango cha elimu katika
mkoa wa Ruvuma ni mbaya hususan kwa shule za sekondari, hivyo kuna kila sababu
kuhakikisha kwamba mkoa huo unajipanga upya katika kutatua tatizo hilo.
No comments:
Post a Comment