Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, Juma Mpeli. |
Na Kassian Nyandindi,
Ruvuma.
SERIKALI wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, imepongezwa kwa
jitihada zake za kudhibiti biashara haramu ya magendo ya kahawa iliyokuwa
ikifanyika wilayani humo na wafanyabiashara wajanja, na kuwasababishia wakulima
wa zao hilo washindwe kusonga mbele kimaendeleo.
Juu ya udhibiti huo, imeelezwa kuwa hivi sasa wakulima
wataweza kuuza kahawa yao kwa bei nzuri na kuwafanya waweze kuwa na kipato na
hata wilaya, kuweza kukusanya mapato yake kwa urahisi.
Hayo yalisemwa na Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)
wilayani Mbinga mkoani humo, Juma Mpeli alipokuwa akizungumza na waandishi wa
habari ofisini kwake.
Alisema Halmashauri kuu ya chama hicho hapa wilayani,
imepokea taarifa kutoka kwa uongozi wa wilaya ya Mbinga juu ya mipango
waliyonayo ya kilimo cha zao la kahawa, na kuunga mkono jitihada hizo ambazo zinaendelea
kufanywa ikiwemo suala hilo la kudhibiti utoroshwaji wa zao la kahawa.
Mpeli alifafanua kuwa CCM hivi sasa imejiwekea mikakati ya
kupita katika kila kata kuhamasisha wakulima, kuuza kahawa yao kwenye vyama vya
ushirika na kazi hiyo itaanza kufanyika mapema mwanzoni mwa mwezi Mei mwaka
huu.
“Sisi kama chama cha mapinduzi tunaipongeza sana serikali
yetu hapa wilayani, kwa hatua hizi walizozichukua katika kudhibiti tatizo hili sugu
ambalo lilikuwa linafanywa na wafanyabiashara ambao hawa watakii mema wakulima
wetu”, alisema.
Pia aliwataka wakulima kuacha biashara ya kahawa mbichi
ambayo huuzwa kwa njia ya magendo, huku akisisitiza ukoboaji ufanywe katika
mitambo ili waweze kupata kahawa iliyokuwa bora na yenye bei nzuri mnadani.
Kadhalika aliongeza kuwa hivi sasa katika msimu wa mavuno ya
zao hilo uonjaji wa kahawa utafanyika hapa Mbinga, badala ya Moshi na zao hilo
kibiashara kuitwa X – Mbinga tofauti na miaka ya nyuma lilikuwa likiitwa X –
Makambako kutokana na kuhifadhiwa katika maghala ya Makambo mkoani Iringa,
ambako hata uzalishaji wa kahawa haupo.
Pamoja na mambo mengine akizungumzia msimamo wa chama hicho,
Mpeli aliwaeleza waandishi wa habari kuwa hivi sasa wamekuwa na mambo matatu
ambayo chama kinasimamia hapa wilayani Mbinga ambayo ni msimamo juu ya muundo
wa katiba, uchaguzi wa serikali za mitaa ambao unatarajiwa kufanyika hivi
karibuni pamoja na sherehe za kuzaliwa kwa chama hicho ambazo zitafanyika
kitaifa mwakani hapa mkoani Ruvuma.
Katibu huyo alisema msimamo wao ni kuwa na serikali mbili na kufafanua
kuwa, hata katika kuzihudumia ni rahisi tofauti na kuwa na serikali tatu ambayo
aliita ni tegemezi na itakuwa mzigo kwa taifa.
Hata hivyo alitoa wito kwa wanachama wa chama hicho watulie,
wasikilize na kufuata misimamo ya chama huku akiongeza juu ya suala la uchaguzi
wa serikali za mitaa nalo wazingatie matakwa ya chama kwa faida ya Watanzania
wote.
No comments:
Post a Comment