Friday, April 11, 2014

AGIZO LA WAZIRI TAMISEMI LA PUUZWA NJAMA ZAUNDWA KUWAREJESHA MADARAKANI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete.




















Na Kassian Nyandindi,

Ruvuma.


OFISI ya Katibu tawala mkoa wa Ruvuma na Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani humo, zimeshushiwa shutuma nzito kufuatia kudaiwa kupuuza na kutotekeleza kwa haraka agizo lililotolewa na Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Ofisi ya waziri Mkuu Tawala za mikoa na Serikali za mitaa (TAMISEMI) Kassim Majaliwa, Mwandishi wetu amebaini.

Uchunguzi umebaini kuwa shutuma hizo zimetolewa baada ya kuonekana wazi kuwa kumekuwa na mchezo mchafu ambao unaendelea sasa, wa kutaka kutengua agizo hilo lililotolewa na Waziri huyo Februari 7 mwaka huu, juu ya kuvuliwa madaraka kwa baadhi ya viongozi wa idara ya elimu sekondari wilayani humo.

Uamuzi wa Serikali wa kumvua madaraka kwa kumshusha cheo aliyekuwa Ofisa elimu Sekondari Hanji Yusuph Godigodi na wenzake sita ambao ni walimu wakuu wa shule za sekondari, ulifuatia kushindwa kutekeleza majukumu yao ya kazi na kufanya ubadhirifu wa zaidi ya shilingi milioni 268 za maendeleo ya elimu ya sekondari wilayani humo.

Fedha hizo zilizotafunwa zililenga kufanya kazi ya kununua vitabu kwa shule za sekondari wilayani Mbinga, lakini inashangaza kuona kwamba utekelezaji husika kama serikali ilivyopanga haukufanyika.

Katika fedha hizo shilingi milioni 108 ilibidi zitumike kununua vitabu hivyo, na zinazobakia zifanye shughuli zingine za maendeleo husika katika shule hizo.


Wakuu wa shule za sekondari wilayani Mbinga ambao walishushwa madaraka ni William Hyera ambaye ni wa shule ya sekondari Maguu, Clemence Sangana anatoka shule ya sekondari Mkuwani, Method Komba Langilo sekondari, John Tillia Ukilo sekondari, Leonard Juma Luli Sekondari huku akimtaja kwa jina moja mwalimu Konga ambaye yupo sekondari ya Kihangimahuka.

Katibu tawala wa mkoa wa Ruvuma Hassan Bendeyeko anadaiwa kupanga njama kwa kushirikiana na Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga Hussein Ngaga, za kuwarejesha madarakani watumishi hao ambao kimsingi walikwisha vuliwa madaraka na Waziri Majaliwa alipokuwa katika ziara yake ya  kikazi wilayani Mbinga.

Bendeyeko na Ngaga wameonyesha dhahiri kwamba lengo lao la kupuuza agizo hilo lililotolewa na serikali, ni baada ya kuunda tume ya watu watatu kutoka Ofisi ya Katibu tawala huyo ambayo imepewa kazi ya kuwahoji walimu wakuu wa sekondari wilayani humo kazi ambayo imeanza kufanyika mapema Aprili 5 mwaka huu na sasa bado inaendelea.

Mtandao huu umepata majina ya tume hiyo inayoongozwa na Mwenyekiti wake Humphrey Paya ambaye ni Msaidizi wa katibu tawala wa mkoa huo idara ya utumishi na wajumbe wenzake wawili ambao ni Frazier Zombe, afisa elimu taaluma mkoa wa Ruvuma na Zaina Mzindakaya Mweka hazina Halmashauri ya wilaya ya Namtumbo.

Kadhalika imebainika kuwa tume hiyo ambayo imeundwa bila kufuata taratibu husika na wala kuhusishwa viongozi wengine wa halmashauri ya wilaya ya Mbinga akiwemo Mwenyekiti wake wa halmashauri ya wilaya hiyo Allanus Ngahy, inadaiwa kusababisha kuzua malalamiko makubwa kutoka kwa baadhi ya Madiwani ambao ni wajumbe wa kamati ya fedha katika kikao chao walichoketi leo Aprili 11 mwaka huu na kumuagiza Mwenyekiti huyo kuhakikisha haraka iwezekanavyo azungumze na Mkurugenzi wake kwa nini amefanya hivyo bila kushirikisha uongozi husika na kutolea majibu haraka iwezekanavyo kwa kamati hiyo.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti Madiwani hao wameonesha kusikitishwa na kulalamikia kitendo hicho kilichofanywa na Bendeyeko kwa kushirikiana na Ngaga, kwani kinaonesha wazi ni utovu wa nidhamu na ukiukwaji wa maadili ya utumishi wa umma ukizingatia kwamba agizo hilo lilikwisha tolewa na kiongozi wa ngazi ya juu serikalini.

“Sisi inatushangaza kuona tume hii ipo hapa bila taarifa rasmi huku ikilipwa fedha (posho) ambazo kimsingi zilipaswa kusaidia shughuli nyingine za maendeleo ya wananchi wetu”, walisema.

Kadhalika Walimu wakuu wa shule za sekondari wilayani Mbinga ambao wameitwa na kuhojiwa na tume hiyo, nao wameshangazwa na kitendo hicho ambapo wamesema hawaoni sababu ya msingi ya wao kuitwa kuja kuhojiwa juu ya ubadhirifu wa fedha hizo shilingi milioni 268 za maendeleo ya elimu ya sekondari wilayani humo, ambazo walikwisha tolea majibu kufuatia ukaguzi uliofanyika na Mkaguzi wa ndani wa halmashauri ya Mbinga.

Walisema inawashangaza kuona wanaitwa kwa kupigiwa simu huku wengine wakitumiwa ujumbe wa meseji kwamba wanatakiwa kuja makao makuu ya wilaya hiyo, kwa ajili ya kuhojiwa kuhusiana na suala hilo ambalo awali tayari lilikwisha fanyiwa kazi.

Walimu hao walilalamikia pia kutumia gharama kubwa ya kuja makao makuu ya wilaya hiyo, bila kurejeshewa gharama za usumbufu jambo ambalo walisema ni kinyume cha utaratibu kwani wamekuwa wakiishi mazingira magumu mjini hapa, na kwamba walipouliza kwa uongozi husika juu ya kama kuna malipo ya kurejeshewa gharama za usumbufu waliambiwa hakuna.

“Hata kulala tunajitegemea tumeweka madeni katika nyumba za kulala wageni, sisi hatujafurahishwa juu ya mwenendo wa suala hili”, walisema.

Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga Ngaga alipoulizwa ofisini kwake alikiri kuwepo kwa tume hiyo huku akipinga kuundwa na Ofisi ya Katibu tawala wa mkoa huo, na kueleza kuwa yeye ndiye aliyeiunda.

“Mimi ndiye niliyeunda tume unajua sikutaka kutumia watu wa hapa nikaona vyema nitumie watu wa mkoani, huyu afisa elimu sekondari anatuhuma nyingi inatubidi tufanye hivi kwanza licha ya tamko la Waziri kuwepo lakini maamuzi yaliyotolewa na Waziri yatabaki palepale,

“Unajua nikueleze hauwezi kujua ukaribu wa huyu mtu na ofisi ya RAS upoje naomba mliache kwanza tupo tunalifanyia kazi litakwisha tu’,  alisema Ngaga.

Alipohojiwa Katibu tawala wa mkoa wa Ruvuma Bendeyeko kwa njia ya simu alisema yeye hawezi kuzungumzia lolote yupo safarini.

“Kama ulikuwa unanipigia simu kwa muda mrefu usingeweza kunipata niliifunga kwa muda na hivi sasa nipo eneo la mikumi……. hatuwezi kuzungumza”, alisema Bendeyeko.













 





No comments: