Na Kassian Nyandindi,
Songea.
WANAFUNZI wa shule ya sekondari ya Village
School of Tanzania (VST) iliyopo katika kijiji cha Unango wilayani Mbinga mkoa
wa Ruvuma wamefanya fujo kwa kumpiga mkuu wao wa shule, na kuvunja baadhi
ya samani za shule hiyo huku wakisababisha uharibifu mkubwa wa mali za shule na walimu wao.
Kamanda wa Polisi wa mkoa huo Akili
Mpwapwa alisema kuwa tukio hilo limetokea mwishoni mwa wiki
iliyopita majira ya saa za usiku katika kijiji hicho.
Alisema kuwa siku hiyo ya tukio
wanafunzi wa kidato cha tatu na nne wa shule hiyo walifanya fujo na
kusababisha mali za shule pamoja na za walimu wao kuharibiwa ambapo
nyumba mbili za walimu zilivunjwa milango na madirisha.
Wanafunzi hao walivunja
kompyuta na kuchana vitabu mbalimbali na nguo za walimu wao na kusababisha
fedha shilingi milioni mbili kupotea.
Uharibifu huo wa miundombinu ya
shule pamoja na mali imeelezwa kufikia thamani ya shilingi milioni 17,680,000
na kwamba bado uongozi wa shule unaendelea kuangalia hasara zaidi
zilizojitokeza.
Kamanda Mpwapwa alibainisha kuwa sababu
ya wanafunzi hao kufanya vurugu shuleni hapo ni kwamba mkuu wa shule hiyo
Angelo Malaki aliwazuia kufanya sherehe za kuwakaribisha wanafunzi wenzao
wa kidato cha kwanza, wakati tayari walishachangishana fedha
ambazo walimkabidhi mkuu huyo wa shule kwa
ajili ya maandalizi ya sherehe hiyo.
Kufuatia kwa vurugu hizo imelazimika
uongozi husika wa shule hiyo kuifunga kwa muda wa wiki mbili na wanafunzi wote
wamerudishwa majumbani kwao, kupisha uchunguzi zaidi ili kubaini chanzo halisi
cha tukio hilo na mpaka sasa hakuna mwanafunzi yoyote anayeshikiliwa na polisi.
Baadhi ya wanafunzi wa shule ya sekondari ya VST ambao majina yao waliomba yahifadhiwe walisema kabla ya kutokea vurugu hizo wanafunzi walichangishana fedha shilingi laki saba, kwa ajili ya sherehe fupi za kuwakaribisha wanafunzi wenzao wa kidato cha kwanza na fedha hizo alikabidhiwa mkuu wa shule Angelo Malaki na walipomtaka mkuu wa shule apange tarehe ya kufanya sherehe hizo aliwalazimisha wafanye katikati ya wiki wakati wanafunzi wenyewe walitaka wafanye siku ya jumamosi, ambayo mkuu huyo wa shule alikataa kwa madai kuwa yeye ni msabato hawezi kuruhusu shughuli hiyo ifanyike siku hiyo jambo ambalo lilianza kuzua mvutano.

Kwa upande wake Mkuu wa wilaya
ya Mbinga Senyi Ngaga amethibitisha kutokea kwa vurugu hizo na kusema hatua za
awali zimeanza kuchukuliwa, kupitia vikao mbalimbali vya kamati ya shule pamoja
na kamati ya maendeleo ya kata hiyo ili kuweza kupata ufumbuzi wa chanzo
cha vurugu hizo.
No comments:
Post a Comment