Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
ASKOFU wa Jimbo Katoliki la Mbinga mkoani Ruvuma John Ndimbo,
amewataka Madiwani wa wilaya ya Mbinga mkoani humo kuacha itikadi za kisiasa
pale wanapotekeleza mambo ya msingi ya wananchi, na endapo wasipozingatia hilo
huenda wakasababisha machafuko katika jamii.
“Mwanasiasa yeyote ambaye hana kanuni na hazingatii mambo ya
msingi huyo anaipoteza jamii, tuache itikadi za kisiasa tutekeleze kwanza majukumu
tuliyopewa na wananchi”, alisema Ndimbo.
Kauli hiyo ilitolewa na Askofu huyo katika kikao cha
tathimini ya elimu kilichoketi hivi karibuni, kwenye ukumbi wa jimbo katoliki
la Mbinga ambacho kilikuwa kikiendeshwa na Mwenyekiti wake Mkuu wa wilaya hiyo
Senyi Ngaga.
Ndimbo alisema lengo la kikao hicho ni kutaka kuboresha masuala
ya elimu wilayani Mbinga, hivyo wanasiasa na watendaji husika katika sekta
mbalimbali wilayani humo, hawana budi kujenga ushirikiano ili kumpiga vita adui
ujinga ambaye bila elimu hakuna maendeleo.
“Nawasihi katika elimu tusifanye siasa, popote pale penye
mafanikio ni lazima pawepo na jitihada ambayo inafanyika”, alisisitiza.
Aidha alieleza kuwa wanasiasa kuendelea kupigana vijembe
majukwaani au katika vikao mbalimbali, wadau wa elimu wanavunjika moyo badala
yake kila mtu atimize wajibu wake na sio kuingiliana katika majukumu ya kazi.
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Mbinga Ngaga,
alisema wilaya hiyo imejiwekea mikakati kabambe kwamba suala la elimu linapewa
kipaumbele kwanza katika kuhakikisha mambo ya msingi yanatekelezwa ipasavyo,
kwa kuhakikisha sekta hiyo inasonga mbele kwa faida ya kizazi cha sasa na
kijacho.
No comments:
Post a Comment