Askofu mkuu Damian Dallu wakati akitoa mahubiri katika maadhimisho
hayo kwa waumini wa kanisa Katoliki (hawapo pichani) Parokia ya Mbangamao Jimbo
la Mbinga mkoani Ruvuma. (Picha zote na Julius Konala)
Na Julius Konala,
Mbinga.
ASKOFU mkuu Damian Dallu, wa Jimbo kuu Katoliki la
Songea mkoani Ruvuma ameipongeza Parokia ya Mbangamao iliyopo katika Jimbo la
Mbinga mkoani humo, kwa mchango wake mkubwa wa kusukuma maendeleo hususani
katika sekta ya elimu kwa kipindi cha miaka 50 tangu kuanzishwa kwake mwaka
1964 chini ya Paroko wake wa kwanza mzalendo Hayati Askofu Maurus Komba.
Askofu Dallu ametoa pongezi hizo wakati akiwahubiria mamia ya Waumini wa kanisa hilo kwenye maadhimisho ya Ibada ya misa takatifu ya shukrani,
Jubilei ya miaka 50 ya parokia hiyo iliyofanyika nje ya viwanja vya kanisa hilo
na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo maaskofu, mapadre, watawa, waumini
pamoja na viongozi wa serikali.
Alisema Parokia hiyo kupitia Shirika la Wavisenti imefanikiwa
kupanua wigo mkubwa wa kutoa huduma kwa jamii, ikiwemo kuongeza idadi ya shule
za msingi hadi kufikia 15, shule za sekondari tatu na ujenzi wa shule za
chekechea kwa kila kigango.
Vilevile ameeleza kuwa wameweza kutoa huduma ya maji safi na
salama kwa wakazi wa eneo hilo ikiwemo pamoja na parokia hiyo kuzaa parokia
mpya ya Mpepai iliyopo wilayani humo na kufanya ukarabati wa zahanati, shule za
msingi na ujenzi wa sekondari.
Hata hivyo amewaomba waumini wa kanisa Katoliki kuliombea
Taifa ili liweze kuendesha mchakato wa uundaji wa katiba mpya, uchaguzi ujao wa
serikali za mitaa pamoja na uchaguzi mkuu wa Wabunge na Rais katika hali ya amani
na utulivu tuliyoachiwa na muasisi wa taifa hili Hayati, Mwalimu Julius Kambarage
Nyerere.
Waumini hao wameaswa kujenga utamaduni wa kulitegemeza kanisa
kwa kuchangia shughuli za maendeleo ikiwemo ujenzi wa makanisa, uanzishaji wa vigango,
parokia kulipa zaka kwa wakati ikiwemo michango mbalimbali na kuwasaidia
Mapadre badala ya kutegemea wafadhili toka nchi za nje.
Akizungumzia kwa upande wa kiroho Askofu Dallu amesema kuwa
katika kipindi hiki cha miaka 50 ya uinjilishaji Parokia hiyo, pia imefanikiwa
kuongeza idadi ya vigango toka sita na kufikia tisa, ikiwemo pia ongezeko la
idadi ya waumini pamoja na ukomavu wa imani.
Pamoja na mambo mengine ametoa wito kwa mapadre kujenga mazoea
ya kutembelea jumuiya ndogondogo kwa ajili ya kuhamasisha wapagani kurudi
kundini, waumini wanaoishi uchumba kufunga ndoa, pamoja na kuweka utaratibu wa
kutengeneza bajeti ya miezi mitatu katika parokia zao ikiwa ni lengo la
kuimarisha na kurahisisha utendaji wao wa kazi za kila siku.
Kwa upande wake uongozi wa Parokia ya Mbangamao wilayani
Mbinga umesema wamejiwekea mikakati mbalimbali kwa ajili ya kuongeza pato la
Parokia hiyo ikiwemo kuanzisha shamba la Mahindi, kahawa, miti, ufugaji wa kuku
pamoja na kuhakikisha wanapunguza tatizo la watu kuishi katika hali ya upagani
na uchumba.
|
No comments:
Post a Comment