Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
DEREVA
aliyetokomea kusikojulikana ambaye alisababisha ajali ya gari
kutumbukia katika korongo, watu sita kufariki dunia na 18 kujeruhiwa vibaya, waliokuwa
wakisafiri kwa basi kutoka Mbinga mjini kwenda wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma,
amejitokeza na kujisalimisha mikononi mwa Jeshi la Polisi akiwa katika hali mbaya.
Kamanda
wa Polisi wa mkoa huo Mihayo Msikhela amemtaja dereva huyo kuwa ni Paul Nchimbi
(31) mkazi wa kijiji cha Liparamba wilayani Nyasa, ambapo wakati anajisalimisha
mwili wake umejaa majeraha.
Mihayo
alifafanua kuwa baada ya dereva huyo kupatikana kwa hiari yake na kuripoti katika
kituo kikuu cha polisi wilaya ya Mbinga amepelekwa kwa ajili ya kupewa
matibabu, hospitali ya wilaya hiyo huku akiwa chini ya ulinzi mkali.
Alisema
atakapomaliza kupatiwa matibabu na kupona, jeshi hilo litafanya mahojiano naye
ili kuweza kujua chanzo cha tukio hilo ambalo limesababisha baadhi ya Watanzania,
waliokuwa wakisafiri katika basi alilokuwa akiendesha lenye namba za usajili T
759 BVR aina ya Nissan Civillian mali ya Dismas Ndomba mkazi wa kijiji cha
Kingirikiti wilayani wilayani humo, kupata ajali katika kijiji cha Burma majira
ya saa 10:30 jioni Agosti Mosi mwaka huu.
Pamoja
na mambo mengine Mganga mfawidhi wa hospitali ya wilaya ya Mbinga Elisha Robert,
alipozungumza kwa njia ya simu na mwandishi wa habari hizi alisema majeruhi
wote ambao wamelazwa katika hospitali hiyo wanaendelea vizuri isipokuwa wagonjwa wanne wamesafirishwa kwenda
hospitali ya Peramiho, iliyopo wilaya ya Songea mkoani humo kutokana na kuwa
katika hali mbaya.
“Vilevile
tumesafirisha wagonjwa wengine wawili wameenda kupatiwa matibabu hospitali ya
misheni Litembo iliyopo huku Mbinga hali zao sio nzuri wamevunjika nyonga, tukaona
ni vyema wapelekwe kwanza huko kwa uchunguzi zaidi wa afya zao”, alisema Dokta
Elisha.
Awali
Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Ruvuma Bw. Mihayo alifafanua kuwa ajali hiyo
ilisababishwa na gari kuwa katika mwendo kasi, ambapo dereva aliyekuwa
akiliendesha alishindwa kulimudu kwenye kona kali na hatimaye lilitumbukia
katika shimo kubwa (korongo) na kusababisha mauaji na majeruhi hao.
No comments:
Post a Comment